Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi isiyo kuwa ya Kiserikali ya Utu Wangu Organization (UWO) Fatuma Mgeni, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mjini hapa jana kuhusu kuanzishwa kwa Asasi hiyo yenye makao makuu yake mkoani Singida.
Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi isiyo kuwa ya Kiserikali ya Utu Wangu Organization (UWO) Fatuma Mgeni, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) huku akionesha mguu uliojeruhiwa katika ajali aliyoipata Kibaha kwa Mathias mkoani Pwani Desemba 5, 2018.
Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi isiyo kuwa ya Kiserikali ya Utu Wangu Organization (UWO) Fatuma Mgeni,akifanya mazoezi ya kutembea akiwa nyumbani kwake Singida.
Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi isiyo kuwa ya Kiserikali ya Utu Wangu Organization (UWO) Fatuma Mgeni, akionesha cheti cha usajili wa Asasi yake ya Utu Wangu Organization (UWO) kwa waandishi wa habari.
Na Dotto Mwaibale, Singida.
WAHANGA wa ajali hapa nchini ambao wanakosa huduma baada ya kutelekezwa ama kutokuwa na ndugu wataanza kupatiwa msaada wa hali na mali kutoka Asasi isiyo kuwa ya Kiserikali ya Utu Wangu Organization (UWO) yenye makao makuu yake mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi hiyo Fatuma Mgeni ambaye ni mhanga wa ajali na Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Mkoa wa Pwani, Mkufunzi, Mwamuzi na Kocha wa Mchezo wa Mpira wa Meza (Table Tennis) ngazi ya kwanza ya Dunia, alisema jamii bado ipo nyuma kusaidia wahanga wa ajali ambao wanakosa msaada na kuiachia Serikali ambayo ina majukumu mengi.
“Suala la kuwasaidia wahanga wa ajali lipo ndani ya uwezo wa wanajamii wenyewe kikubwa ni jamii kuhamasika na kuwa na moyo wakusaidia wahanga hao” alisema Mgeni.
Alisema lengo la kuanzisha asasi hiyo ni baada ya kupata ajali Kibaha kwa Mathias na kujeruhiwa vibaya mguu wake wa kulia na kukaa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi Kibaha karibu mwaka mmoja tangu Desemba 5, 2018 hadi leo akipatiwa matibabu ingawa yupo nje ya hospitali.
Mgeni alisema akiwa hospitalini ndipo aliona changamoto ya maisha ya wahanga wa ajali ambao walikuwa hawana msaada baada ya kutelekezwa na jamaa zao na wengine kutokuwa na ndugu kabisa licha ya kupatiwa matibabu.
“Niliguswa na jambo hili nikaona nianzishe asasi hii kwa ajili ya kutoa matumaini kwa wahanga hao kwa kushirikiana na jamii ikiwa ni kumuunga mkono Rais Dkt.John Magufuli za kuboresha huduma katika sekta ya afya na kuhakikisha wahanga hao wanapata haki zao kutokana na majanga walioyapata na kuwa na afya bora ili waweza kurudi katika afya zao za zamani na kuweza kufanya shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wao binafsi na Taifa kwa ujumla.” alisema Mgeni.
Mgeni alisema kumekuwa na dhana potofu kuwa wahanga wa ajali ni lazima wasaidiwe mahitaji yote na Serikali wakati kumbe jamii ikielimishwa inaweza kuwa sehemu ya kutoa faraja kwa wahanga hao kwa kupambana na changamoto zao kuanzia pale wanapopata ajali mpaka kupona kwao wakiwa wazima au na ulemavu uliotokana na ajali.
Aidha Mgeni alisema changamoto kubwa iliyopo ni kwa jamii kuwa nyuma katika jambo hilo ambapo imefikia baadhi ya watu kuwatelekeza wagonjwa hospitali na majumbani na kuwaacha wakiteseka na kukosa matumaini ya maisha.
Alisema kupitia Shirika hilo ambalo limesajiliwa na litakuwa likifanya kazi mikoa yote Tanzania Bara litakuwa likijihusisha zaidi kwa ajili ya kuhamasisha jamii kwa ajili ya kuwasaidia wahanga hao wa ajali.
Mgeni alitumia nafasi hiyo kuwa pongeza madaktari na wauuguzi na wafanyakazi wote wa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi Kibaha kwa jitihada zao kubwa za kitabibu wanazo zitoa kwa jamii hasa kwa watu wanaofikishwa katika hospitali hiyo baada ya kupata ajali kwa kuwapa matibabu kwanza bila ya kuwadai fedha na kuwa ana amini hata hospitali zingine hapa nchini zinafanya utaratibu huo.