**********************************
Na Mwandishi wetu, Hanang`
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara kwa tiketi ya CCM, mhandisi Samwel Hhayuma amewasilisha changamoto zinazoikabili Jimbo hilo kwa mgombea mwenza wa urais Samia Suluhu Hassan.
Mhandisi Hhayuma alitoa changamoto hizo wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika mji mdogo wa Katesh.
Alitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo ni ubovu wa miundombu ya barabara, maji na nishati ya umeme vijijini.
Alisema wanaomba kujengewa kilomita 10 ya barabara ya lami kwenye mji mdogo wa Katesh na lami kutoka kata ya Mogitu hadi hospitali ya kilutheri ya Haydom wilayani Mbulu.
Alisema changamoto za maji zinawakabili wananchi wa vijiji mbalimbali ikiwemo kutokamilika mradi wa maji wa thamani ya sh2 bilioni wa kutoka kata ya Mogitu hadi mji mdogo wa Katesh.
“Pia kuna changamoto ya nishati ya umeme kwani ni asilimia 75 pekee ya vijiji vya jimbo la Hanang’ ndiyo kuna umeme bado asilimia 25 ya vijiji ambavyo havina umeme,” alisema mhandisi Hhayuma.
Hata hivyo, mgombea mwenza huyo Samia alisema kupitia ilani ya uchaguzi wa CCM changamoto nyingi zilizotajwa na mhandisi Hhayuma zitapatiwa ufumbuzi kwa kutekelezwa kwa mwaka 2020/2025.
Alisema miradi ya maji itakamilishwa, umeme utafika vijiji vyote na barabara ya lami ya Mogitu hadi Haydom itajengwa kwani ipo kwenye ilani ya uchaguzi kwa mwaka 2020/2025.
“Ili kukamilisha hayo tunaomba muichague CCM kwa kumpa kura nyingi Rais John Magufuli, mhandisi Hhayuma na madiwani wanaotokana na CCM,” alisema.
Waziri mkuu mstaafu Fredrick Sumaye alisema mhandisi Hhayuma ni kijana msomi ambaye anaweza hata kuchaguliwa kuwa waziri pindi akichaguliwa kuwa mbunge na Rais Magufuli atakaposhinda tena.
Sumaye alisema wananchi wa Hanang’ wasipotoshwe na wapinzani na kupoteza kura zao kwani muda wa siasa umeshapita kimachotakiwa ni maendeleo pekee.
Mbunge wa jimbo hilo wa kipindi kilichopita, Dkt Mary Nagu alisema mradi wa maji wa Mogitu hadi Katesh wa gharama ya sh2 bilioni umechukua muda mrefu bila kukamilika.
“Maji ni uhai na inabidi mradi huu uelekezewe nguvu zaidi ili uweze kukamilika na wananchi wa eneo hili la Katesh wapate maji ya uhakikika,” alisema Dk Nagu.
Mshindi wa ubunge wa jimbo hilo kupitia kura za maoni ya chama hicho, George Bajuta alisema wanaosema amenuna baada ya jina lake kukatwa ni waongo kwani anaunga mkono uamuzi wa CCM kwa asilimia 100.
“Baba yako akiamua mwingine akachunge ng’ombe hupaswi kulalamika kazi zipo nyingi huenda nikatumwa kuuza duka au nikapewa kazi nyingine,” alisema Bajuta.