Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewapa miaka hamsini wapinzani kujijenga kuwa taasisi imara zinazoweza kushindana na CCM kwa sera na kiuongozi.
Ameyasema hayo leo tarehe 01 Oktoba, 2020 katika mkutano wa kampeni uliyofanyika Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein.
“Msimamo wetu ni kuendesha siasa safi na kampeni za ustaarabu, msimamo wetu ni kusimamia haki ya kujitawala kama taifa huru, kwa sababu haki zote msingi wake ni uhuru wetu, mapinduzi yetu na muungano wetu. Hatutachokozeka.”
Akieleza namna baadhi ya vyama vya siasa vinavyoendesha kampeni zisizo za kistaarabu, Katibu Mkuu amesema, “..Dawa yao ni kuwashinda, wachague njia matatu kati ya, kusalimu amri na kurudi CCM, pili, Wastaafu siasa na wafaidike na Ilani ya CCM wapate pensheni, njia ya tatu ngumu sana ni kuunda vyama imara vya kushindana na CCM, hiyo ni njia ngumu lakini ni muhimu kwao na inaweza ikawachukua miaka hamsini kufika hatua hiyo”.
Aidha, Katibu Mkuu ameahidi kuwa, CCM itaendelea kuzisimamia serikali zake zote mbili kuendelea kusimamia maslahi ya wazee wote nchini.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo, wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, Viongozi wa Mkoa, na viongozi mbalimbali wa wilaya zote za mkoa wa Kusini Unguja wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalah Juma Saadala (Mabodi).