Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde akieleza jambo wakati wa kikao cha pamoja na Maafisa Ushirika pamoja na Viongozi wa Vyama vya Ushirika Mkoani Lindi
Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Lindi Edmund Massawe akifafanua suala la Ushirika katika kikao cha pamoja cha maandalizi ya msimu wa Korosho kwa Maafisa Ushirika pamoja na Viongozi wa Ushirika Mkoani Lindi.
Meneja wa Chama cha Ushirika cha RUNALI Jahida Hassan akichangia mada wakati wa kikao cha pamoja cha maandalizi ya msimu wa Korosho kwa Maafisa Ushirika pamoja na Viongozi wa Ushirika Mkoani Lindi.
………………………………………………………………………………………….
Uhakiki wa taarifa za Wakulima wa Vyama vya Ushirika umetajwa kuwa ni moja ya suala muhimu litakalosaidia katika kuwatambua wakulima ili kusaidia katika upatikanaji wa huduma mbalimbali hususani taarifa za akaunti za Benki kwaajili ya malipo ya wakulima.
Hayo ni miongoni mwa mambo aliyosisitiza Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde alipokuwa akiongea na Maafisa Ushirika wa Wilaya za Mtama, Ruangwa, Nachingwea, Kilwa pamoja na Viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Lindi Mwambao pamoja na Runali Mkoani Lindi wakati wa kikao cha pamoja cha kutathmini na kujadili masuala ya Ushirika.
Naibu Mrajis ameshauri Maafisa Ushirika kusaidia kufuatilia maandalizi muhimu katika Vyama vya Ushirika yanafanyika kwa usahihi hususani wakati wa misimu ya mazao kama ambavyo hivi sasa tunapoelekea katika msimu wa Korosho. Akitaja baadhi ya maandalizi hayo ni pamoja na kuwakumbusha na kuwaomba Wakulima kuhakiki taarifa zao za majina kwenye Vyama vyao vya Ushirika pamoja na Mabenki ili taarifa hizo zinapokuwa sahihi zitasaidia wakulima kulipwa kwa wakati na kuondokana na malalamiko.
“Ni wazi kuwa taarifa za Wakulima zinapokuwa hazipo sahihi lazima malipo yatachelewa kuwafikia na hata wengine kutowafikia, nitoe wito kwa Maafisa Ushirika kutoa elimu na kusimamia taarifa na Kanzidata za Wakulima kwenye Vyama zinakuwa sahihi,” alisisitiza Naibu Mrajis
Aidha, ameongeza kuwa Maafisa Ushirika kwa kushirikiana na Viongozi wa Vyama watoe taarifa pale wanapoona kuna dosari zozote zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu huku akiwataka Maafisa hao kuangalia hali za Mizani zilizopo katika Vyama na Maghala kama sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa zao la Korosho 2020/21.
“Maafisa Ushirika pale ambapo kuna mizani hazijapimwa na wataalamu toeni taarifa haraka kwa wahusika wa Wakala wa Vipimo ili watusaidie kuweka mizani zetu vizuri,” alisema Naibu Mrajis
Nae Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Rashid Masoud ametoa wito kwa Wakulima katika msimu huu mpya wa Korosho kuzingatia ubora wa zao la Korosho kwa kufuata kanuni na taratibu za ukusanyaji wa Korosho safi, zilizokauka na kuzingatia madaraja kwa mujibu wa maelekezo ya Wataalamu Magahalani.