Msajili Msaidizi wa Watoa Huduma za Kisheria mkoa wa Shinyanga Tedson Ngwale akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa Wasaidizi wa Kisheria kutoka wilayani Kahama yaliyolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijinsia hasa yanayowakumba wanawake na watoto leo Alhamis Oktoba 1,2020. Mafunzo hayo yameandaliwa na Shirika la TGNP na UNFPA kwa kushirikiana na PACESHI. Kulia ni Meneja Mradi wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kupitia Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) John Shija kutoka Shirika la PACESHI Shinyanga mjini, kulia ni Mwezeshaji katika mafunzo hayo,Mwanasheria Neema Ahmed. Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Wasaidizi wa Kisheria wakiwa katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa namna ya kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijisia hasa yanayowakumba wanawake na watoto.
Meneja Mradi wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kupitia Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) John Shija kutoka Shirika la PACESHI Shinyanga mjini akizungumza wakati mafunzo kwa Wasaidizi wa Kisheria kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa namna ya kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijinsia hasa yanayowakumba wanawake na watoto.
Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Mwanasheria Neema Ahmed akizungumza wakati mafunzo kwa Wasaidizi wa Kisheria kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa namna ya kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijinsia hasa yanayowakumba wanawake na watoto.
Mwanasheria Neema Ahmed akitoa mada kuhusu ukatili wa kijinsia
Mwezeshaji katika mafunzo hayo, Annamarie Mavenjina Nkelame akizungumza wakati mafunzo kwa Wasaidizi wa Kisheria kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa namna ya kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijinsia hasa yanayowakumba wanawake na watoto.
Washiriki wa mafunzo wakiwa katika picha ya pamoja
Washiriki wa mafunzo wakiwa katika picha ya pamoja
Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na UNFPA na Shirika la linalotoa msaada wa kisheria mkoani Shinyanga Paralegal Aid Centre (PACESHI), limetoa mafunzo kwa Wasaidizi wa Kisheria kutoka wilayani Kahama ya kuwajengea uwezo wa namna ya kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijinsia hasa yanayowakumba wanawake na watoto.
Mafunzo hayo yatakayodumu kwa muda wa siku tatu kuanzia leo Oktoba 1,2020 yamefunguliwa rasmi na Msajili Msaidizi wa Watoa Huduma za Kisheria mkoa wa Shinyanga Tedson Ngwale katika ukumbi wa Shinyanga Fairies Hoteli Mjini Shinyanga na kukutanisha pamoja Wasaidizi wa kisheria 21 kutoka Halmashauri ya wilaya ya Msalala na Kahama Mji.
Akifungua mafunzo hayo, Msajili Msaidizi wa Watoa Huduma za Kisheria mkoa wa Shinyanga Tedson Ngwale aliwataka Wasaidizi wa Kisheria kutumia ujuzi watakaopewa kwenda kuwahudumia wananchi wa hali ya chini kupata haki zao kwa mujibu wa sheria.
“Nendeni mkahudumie wananchi,wasaidieni kwa kushughulikia kumaliza matatizo ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Sitapendi kuona wala kusikia mnakaa kimya pindi matukio ya ukatili wa kijinsia yanapotokea katika jamii”,alisema Ngwale.
Aidha aliwasihi Wasaidizi wa Kisheria kuepuka vitendo vya rushwa na kuhakikisha wanawahudumia wananchi bure bila kuwatoza fedha ili kuhakikisha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinatokomezwa katika jamii.
“Wasaidizi wa kisheria mna msaada mkubwa ndani ya jamii hasa wale wa hali ya chini, ambapo wanawake na watoto wamekuwa wakitendea vitendo vya kikatili na wamekuwa wakipoteza haki zao kwa sababu ya kutozijua sheria au ukosefu wa fedha za kulipa mawakili, lakini wasaidizi wa kisheria mtawasaidia kupata haki zao mahakamani bila ya kutoa pesa yoyote”,aliongeza Ngwale.
Katika hatua nyingine alimkumbusha Katibu wa Kamati za Ulinzi na Usalama kwa wanawake na watoto halmashauri ya wilaya ya Msalala,mara baada ya mafunzo hayo kuwaingiza Wasaidizi wa Kisheria kwenye kamati kama wajumbe kwa mujibu wa Mwongozo wa Kitaifa wa Kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kupitia Wasaidizi wa Kisheria (Paralegals) John Shija kutoka Shirika la PACESH Shinyanga mjini alisema Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na TGNP na kuratibiwa na PACESHI yamelenga kuwajenga uwezo wa kisheria wasaidizi hao wa kisheria kuhusu namna ya kutoa msaada wa kisheria kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia.
Naye Mwezeshaji katika mafunzo hayo,Mwanasheria Neema Ahmed aliwataka Wasaidizi wa kisheria pindi wanaposhindwa kusuluhisha migogoro ya ndoa wawaelekeze wahusika waende kwenye mabaraza ya usuluhishi wa ndoa, na endapo wakifika huko wakashindwa kupata suluhu watapewa fomu namba 3 kwa ajili ya kwenda makahamani kufungua shauri la talaka.
Nao washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Gridius Gration na Neema John waliishukuru TGNP kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia katika masuala ya ukatili wa kijinsia.