Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akiongea na wadau wa michezo wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya cha jijini Dar es salaam kitakachosaidia kuwaandaa na kuongeza idadi ya wataalamu wa michezo nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali mara baada ya kuzindua Kituo cha Chuo cha Maendeleo ya Michezo cha Malya jijini Dar es salaam ambacho kitakachosaidia kuongeza idadi ya wataalamu wa michezo nchini.
*******************************
Na Eleuteri Mangi, WHUSM
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amezindua kituo cha michezo ili kuwaandaa na kuongeza idadi ya wataalamu wa michezo nchini.
Kituo hicho kinachoendeshwa na cha Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kipo jijini Dar es salaam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo Dkt. Abbasi alibainisha kuwa kati ya mambo ambayo alikuwa anajifunza baada ya kukabidhiwa wizara hiyo ilikuwa ni pamoja na uendeshaji wa shughuli za Wizara na taasisi zake hatua iliyompelekea kuagiza chuo hicho kiboreshwe ili iwe fursa ya kutengeneza wataalamu wa michezo wengi nchini.
“Tumefanya uamuzi mgumu na muhimu sana wa kuleta kituo cha chuo chetu cha Michezo Malya hapa Dar es salaam ili kutoa na kuendeleza elimu ya michezo katika kada zote nchini na tunaamini mahitaji ni mengi sana” alisema Dkt. Abbasi.
Dkt. Abbasi amesema kuwa wameanzisha kituo ambacho kitatoa programu mbalimbali za michezo ili kuendana na hali halisi ya sekta ya michezo na kuwafanya wataalamu wa michezo wakiwemo wachambuzi, walimu wa michezo na waamuzi kuwa na mawanda mapana katika michezo hatua inayosaidia kuendana na hali halisi ya michezo kwa mujibu wa Shirikisho la Michezo Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la duniani (FIFA).
Aidha, Wizara kupitia chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya imesaini Mkataba wa Ushirikiano (MOU) na Shirikisho la Soka nchini (TFF) hatua itakayosaidia kuanzisha na kufundisha programu mbalimbali za michezo zinazoenndeshwa na TFF ili kuleta uhalisia katika uendeshaji wa shughuli za michezo nchini.
Dkt. Abbasi amewasisitiza waajiri, watu binafsi, wachambuzi wa michezo mbalimbali na wadau wa soka na michezo mingine kuwa Kituo cha Malya Dar es salaam katika jijini la kibiashara na kukitumia ili kupata taaluma na ujuzi na kuwa na nchi ya watu wanaosema na kutenda ili kuwa na maendeleo endelevu.
Zaidi ya hayo, Kituo cha Maendeleo ya Michezo Malya cha jijini Dar es salaam kitatoa pia fursa kwa wataalamu wa michezo waliopo jijini humo kushirikiana na chuo hicho ili kuleta tija katika sekta ya michezo.