Migogoro mingi ya ardhi iliyokuwa ikikabili jimbo la Ilemela na kupelekea kukwama kwa baadhi ya shughuli za maendeleo ikiwemo kufanya maendelezo ya ardhi za wananchi kwa asilimia tisini imeweza kutatuliwa kupitia Serikali ya CCM chini ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt John Magufuli.
Hayo yamesemwa na mgombea wa nafasi ya ubunge kwa jimbo la Ilemela kupitia CCM Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akihutubia wananchi wa kata ya Ibungilo katika viwanja vya jirani na Bwalo la Jeshi Nyamanoro ambapo amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake amefanikiwa kusaidia utatuzi wa migogoro mikubwa ya ardhi iliyokuwa ikisumbua wananchi wa jimbo hilo ikiwemo ule wa wananchi na jeshi la polisi katika eneo la Kigoto, kata ya Kirumba, mgogoro wa jeshi la wananchi JWTZ na wananchi wa Lukobe, Buduku kata ya Kahama, mgogoro ardhi kati ya wananchi wa Nyangulukulu na jeshi la wananchi kata ya Ilemela, huku mgogoro wa wananchi na mamlaka ya uwanja wa ndege wa Mwanza ukisubiria maamuzi ya Mhe Rais kwa utatuzi wa mwisho
‘ Suala la migogoro ya ardhi tumelishughulikia kwa zaidi ya asilimia tisini, Migogoro mingi tumeimaliza, Haiwezekani niwe Naibu waziri wa ardhi alaf kwangu kuongoze kwa migogoro ‘ Alisema
Aidha Dkt Mabula akaongeza kuwa mbali na kufanya vizuri katika sekta ya ardhi katika suala la urasimishaji makazi na umilikishaji wa ardhi kwa miaka mitatu mfululizo wilaya ya Ilemela imefanikiwa kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga shule mpya tatu za msingi, shule mpya tatu za sekondari na mpya mbili za kidato cha tano na sita za Sangabuye na Buswelu.
Akimkaribisha mgombea huyo, Meneja kampeni Ndugu Kazungu Safari Idebe akasema kuwa wananchi wa Ibungilo wana kila sababu ya kukipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na kunufaika na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati jimboni humo ikiwemo utoaji wa elimu bure, ujenzi wa hospitali ya wilaya, mradi wa ufuaji umeme wa Mwl Nyerere na ujenzi wa reli ya kisasa.
Nae mgombea udiwani wa kata hiyo Husein Magera akasema kuwa hakuchukua fomu ya kugombea nafasi ya udiwani ili afurahishe watu bali amedhamiria kuwasaidia wananchi wa kata hiyo kwamba changamoto nyingi za wananchi hao anazijua ikiwemo ukosefu wa zahanati kwa mtaa wa Kiloleli ‘A’ na kuahidi ajira kwa Vijana kupitia miradi itakayokuwa inatekelezwa kwa ngazi ya kata.