Wajumbe wa Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo wakikagua miundombinu ya maji katika Shule ya Msingi Makugwa iliyopo katika kijiji cha Mukubu, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera wakiwa katika ziara ya kazi, Septemba 29, 2020. Shule hiyo ni mojawapo ya wanufaika wa miradi ya kijamii inayotekelezwa na Mradi husika ambapo imejengewa vyumba vya madarasa, Ofisi na nyumba za walimu, vyoo vya wanafunzi pamoja na tanki la maji safi. Kutoka kushoto ni Mhandisi Innocent Luoga, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mradi na Kiongozi wa Msafara, Herman Hume, Mratibu wa Miradi ya Maendeleo ngazi ya Wilaya na Mhandisi Costa Rubagumya ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mradi.
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikikagua banda kitalu maarufu kama ‘green house’ kwa lugha ya kigeni lililoandaliwa kwa ajili ya kilimo cha kisasa katika kijiji cha Chivu, Kata ya Ntoreye, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo,
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikikagua mradi wa ufugaji nyuki katika kijiji cha Chivu, Kata ya Ntoreye, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikikagua miundombinu mbalimbali ya karakana ya useremala na ushonaji nguo katika Chuo cha Ufundi Stadi Lemera kilichopo katika kijiji cha Mukibogoye, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo
Bweni la wanafunzi wa Kike katika Shule ya Sekondari Bukiriro, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, lililojengwa kupitia Mradi wa Umeme Rusumo. Taswira hii ilichukuliwa Septemba 29, 2020 wakati wa ziara ya Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi huo, kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi husika.
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikizungumza na wanafunzi katika Shule ya Msingi Makugwa iliyopo katika kijiji cha Mukubu, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo Septemba 29, 2020 ambapo Shule hiyo imenufaika kwa kujengewa vyumba vya madarasa, nyumba na ofisi za walimu, tanki la maji savi na vyoo vya wanafunzi.
Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mradi wa Umeme wa Rusumo unaotekelezwa wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, Mhandisi Costa Rubagumya (kushoto), akizungumza jambo wakati wa ziara ya Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi huo, Septemba 29, 2020. Hapa ni Shule ya Sekondari Bukiriro ambayo ni mnufaika wa Mradi huo. Kulia ni Mjumbe wa Bodi ya Mradi huo, Mhandisi Innocent Luoga na katikati ni Gaspar Mashingia, Afisa Mwandamizi, Jamii, Maendeleo na Uhamaji Makazi.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mradi wa Umeme Rusumo ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (kulia), akimsisitiza Mwalimu Mkuu (kushoto) wa Shule ya Msingi Makugwa iliyopo katika kijiji cha Mukubu, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, kutunza miundombinu iliyojengwa katika shule hiyo. Mhandisi Luoga alikuwa katika ziara ya kazi akiongoza Timu ya Serikali inayosimamia Mradi husika kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi huo
Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mradi wa Umeme wa Rusumo unaotekelezwa wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, Mhandisi Salum Inegeja, akiwa amekaa katika Ofisi ya Walimu, Shule ya Msingi Makugwa iliyopo katika kijiji cha Mukubu, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera. Shule hiyo ni mojawapo ya wanufaika wa miradi ya kijamii inayotekelezwa na Mradi husika ambapo imejengewa vyumba vya madarasa, Ofisi na nyumba za walimu, vyoo vya wanafunzi pamoja na tanki la maji safi. Mhandisi Inegeja ni miongoni mwa wajumbe wa Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi huo, iliyokuwa katika ziara kukagua miradi husika
………………………………………………………………………………..
Veronica Simba – Ngara
Serikali imewaasa wananchi wa Ngara, Mkoa wa Kagera kutunza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kijamii, inayoendelea kutekelezwa wilayani humo kupitia Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera (megawati 80).
Wito huo ulitolewa jana Septemba 29, 2020 na Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi huo ikihusisha Wakurugenzi wa Bodi na Kamati ya Ufundi, wakiwa katika ziara ya kazi yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi husika.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na Maafisa Watendaji pamoja na wananchi katika maeneo mbalimbali kulipo na miradi hiyo, Kiongozi wa Timu hiyo, Mhandisi Innocent Luoga ambaye ni Mjumbe wa Bodi wa Kamati husika, alisema endapo miundombinu hiyo ya miradi husika isipotunzwa, itakuwa ni hasara kwa Serikali na wananchi walengwa.
“Miradi hii inayohusisha shule, vituo vya afya, miradi ya maji, miundombinu ya kilimo na ufugaji bora inalenga kuwanufaisha wananchi, hivyo ili lengo hilo litimie, inabidi itunzwe.”
Timu hiyo ikiwa katika siku ya pili ya ziara yake, ilitembelea miradi kadhaa ikiwemo Shule ya Msingi Makugwa iliyopo katika kijiji cha Mukubu ambayo imenufaika na Mradi huo kwa kujengewa vyumba vya madarasa, Ofisi na nyumba za walimu, vyoo vya wanafunzi pamoja na tanki la maji safi.
Mwalimu Siyajali Manyasi ambaye ni Mkuu wa Shule hiyo aliueleza Ujumbe huo wa Serikali kuwa, kujengwa kwa miundombinu hiyo kumeiwezesha Shule hiyo kupata usajili na kujitegemea kutoka kuwa tawi la Shule ya Msingi Mukubu iliyoko umbali mrefu kutoka hapo.
“Uwepo wa Shule hii umewapunguzia watoto adha ya kutembea mwendo mrefu takribani kilomita 10 kwenda Mukubu na pia uwepo wa majengo haya ya kisasa umevutia wazazi wengi zaidi kuwaleta watoto wao shuleni,” alisema Mwalimu Manyasi.
Vilevile, Timu hiyo ilitembelea Shule ya Sekondari Bukiriro ambayo imenufaika kwa kujengewa bweni la wanafunzi wa kike, bwalo la chakula na vyoo.
Aidha, Ujumbe huo ulitembelea Chuo cha Ufundi Stadi Lemera kilichopo katika kijiji cha Mukibogoye kilichonufaika kwa kujengewa karakana ya useremala na ushonaji nguo pamoja na uwanja wa michezo ambao ujenzi wake unaendelea.
Timu ilitembelea pia miradi ya kilimo cha kisasa kwa njia ya banda kitalu maarufu kama ‘green house’ kwa lugha ya kigeni na mradi wa ufugaji nyuki, inayotekelezwa katika kijiji cha Chivu, Kata ya Ntobeye, yote ikilenga kuwanufaisha wananchi kiuchumi.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mratibu wa Miradi ya Maendeleo ngazi ya Wilaya, Herman Hume alieleza kuwa miradi hiyo ya kijamii inayoendelea kutekelezwa wilayani Ngara ilitengewa fedha kiasi cha dola milioni tano za Marekani ambazo ni sawa na takribani shilingi bilioni 12 za Tanzania.
Kwa upande wao, Mhandisi Salum Inegeja kutoka Wizara ya Nishati na Mhandisi Costa Rubagumya kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mradi wa Rusumo, walikiri kurudhishwa na utekelezwaji wa miradi hiyo lakini wakasisitiza umuhimu wa kuifanya iwe endelevu kwa maslahi ya wananchi.
Katika ziara hiyo, Timu ilifuatana pia na Mhandisi Patrick Lwesya, Meneja Mradi wa Rusumo, Gaspar Mashingia, Afisa Mwandamizi, Jamii, Maendeleo na Uhamaji Makazi pamoja na Maafisa kadhaa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ngara.
Mradi wa Umeme Rusumo unatekelezwa kwa ushirikiano wa nchi tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi ambapo utakapokamilika unatarajiwa kuzalisha megawati 80 za umeme zitakazogawanywa kwa nchi husika.