Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB – Alex Mgeni, akizungumza wakati wa Kongamano la wafanyabiashara ‘NMB Business Club’ Wilaya ya Ilala, lililofanyika katika Ukumbi wa St. Peter’s jijini Dar es Salaam.
Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB – Benedicto Baragomwa akizungumza wakati wa Kongamano la wafanyabiashara la ‘NMB Business Club’ Wilaya ya Ilala, lililofanyika katika Ukumbi wa St. Peter’s jijini Dar es Salaam.
Meneja Mwandamizi Kitengo cha Biashara wa Benki ya NMB – Christopher Mgani, akielezea huduma na bidhaa za NMB wakati wa Kongamano la wafanyabiashara ‘NMB Business Club’ Wilaya ya Ilala.
…………………………………………………………………………………………
Kongamano la wanachama wa Klabu za Biashara ‘NMB Business Club’ Wilaya ya Ilala limefanyika jijini Dar es Salaam, huku Benki ya NMB ikiwaongezea muda wa marejesho ya mikopo wanachama hao, kama unavyotaka mwongozo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akifungua kongamano hilo lililowaleta pamoja zaidi ya wafanyabiashara 100, Mkuu wa Idara ya Biashara wa NMB, Alex Mgeni, alisema wanatambua ugumu wa mazingira ya biashara waliyokumbana nayo wanachama wa klabu za biashara na wateja wao na kwa kuheshimu mwongozo wa BoT, wameamua kuwapa nafuu hiyo ya marejesho.
Hata hivyo, Mgeni alibainisha kuwa licha ya unafuu huo walioutoa, wanashukuru kwa sababu mtiririko wa marejesho kwa wafanyabiashara na wateja wao umeendelea kuwa vizuri, ambako asilimia 80 ya wakopaji wamelipa katika mifumo ya kawaida, jambo linalothibitisha uimara wa mitaji yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Fedha wa NMB, Benedicto Baragomwa, aliwahakikishia washiriki kuwa Benki yake iko imara licha ya mtikisiko wa COVID-19, huku akiitaja siri ya mafanikio hayo kuwa ni uimara wa biashara mzunguko wa fedha wa wateja wao na wanachama wa klabu hizo kote nchini.
Vilevile, Baragomwa aliwapongeza wanachama wa Klabu za Biashara kwa namna walivyopambana na janga la corona, huku akiwataka kuzungumza mara kwa mara na mameneja wa matawi ya NMB yote nchini, kujadili changamoto zinazokwaza biashara zao ili wasikwame.
Kongamano hilo, limetumka kunadi bidhaa mpya za NMB zilizoingizwa sokoni hivi karibuni, za Kadi za Malipo ya Kabla (NMB Pre-Paid Card) na Kadi za Mikopo (NMB Credit Card), sambamba na huduma nyingine kama NMB Nyanyua Mjengo, NMB BancAssurance na NMB Mkononi.
NMB Business Club ni kongamano linalolenga kuwaongezea elimu ya fedha na kubadilishana mawazo wafanyabiashara, sambamba na Benki hiyo kupokea maoni na ushauri wao na kuvifanyia kazi ili kuharakisha maendeleo ya wanachama wake, lakini pia kunadi bidhaa mpya za NMB.