Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Mhe. Gulam Kifu akieleza jambo wakati Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde (hayupo pichani) alipofika Ofisini kwake katika ziara ya kikazi yenye malengo ya ufuatiliaji wa maandalizi ya Mfumo wa Ushirika katika msimu mpya wa Korosho 2020/21
Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde akifafanua jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti wakati wa Ziara ya kikazi yenye malengo ya ufuatiliaji wa maandalizi ya Mfumo wa Ushirika katika msimu mpya wa Korosho 2020/21
Kikao baina ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika kilichoongozwa na Naibu Mrajis Charles Malunde na Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Mhe. Gulam Kifu kujadili masuala mbalimbali ya msimu mpya wa Korosho
Kikao cha Maandalizi ya Mfumo wa Ushirika kilichoongozwa na Naibu Mrajis Charles Malunde kikao kilichohusisha Mrajis Msaidizi Pwani, Maafisa Ushirika wa Wilaya za Mkuranga, Rufiji na Viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Pwani (CORECU) kilichofanyika Wilayani Kibiti
……………………………………………………………………………
Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde amesema ni muhimu kwa kila mmoja katika Mfumo wa Ushirika kuzingatia majukumu yake kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Ushirika hususani kipindi hiki tunapoelekea msimu mpya wa Korosho wa mwaka 2020/21.
Kauli hiyo imetolewa wakati Naibu Mrajis akiongea na Maafisa Ushirika wa Wilaya za Mkoa wa Pwani ikiwemo Mkuranga, Rufiji, pamoja na Viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Pwani (CORECU) kwenye kikao cha maandalizi ya masuala ya Ushirika katika msimu mpya wa Korosho kilichofanyika Wilaya ya Kibiti Septemba 29, 2020.
Akieleza malengo ya kikao hicho Mrajis huyo alifafanua kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na Wadau imechukua jukumu la kuwakutanisha watendaji hao ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu namna bora ya kufanya maandalizi ya kiushirika katika Msimu mpya wa Korosho ili kuhakikisha kuwa kila mmoja katika mfumo huo na Taifa linanufaika kwa kadiri ya malengo yanayotarajiwa.
“Katika msimu huu ni vyema Maafisa Ushirika kuanza kuangalia na kufuatilia mahitaji muhimu yatakayohitajika katika Vyama pamoja na kuainisha changamoto zilizopo au zilizojitokeza msimu uliopita na kuzifanyia kazi na nyingine kuzipeleka katika hatua za juu za utekelezaji ili Mkulima anufaike na kilimo kupitia Ushirika,” amesisiza Naibu Mrajis
Baadhi ya masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa Wakulima wa Korosho kuhusu namna bora za uhifadhi wa Korosho, ukaushaji wa Korosho kabla ya ukusanyaji kwenye Vyama vya Ushirika, wakulima kuwa na Akaunti za Benki kwaajili ya malipo pamoja na masuala ya mahitaji ya vifungashio katika msimu huo.
Katika Hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Mhe. Gulam Kifu amepongeza hatua ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika kufuatilia maandalizi ya Mfumo wa Ushirika katika msimu mpya wa Korosho na kuongeza kuwa misimu ya mazao kama hiyo inaweza kuwa kichocheo cha uanzishaji wa viwanda vya vifungashio nchini. Jambo ambalo linaunga mkono azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Uchumi wa Viwanda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika CORECU Ally Mengesi amesema tayari maandalizi ya awali yameanza na yanaendelea vizuri. Akitaja kuwa Watendaji wa Chama hicho wana mawasiliano ya karibu na Wakulima wa Korosho Mkoani hapo hivyo kusaidia kufikisha ujumbe unaohitajika. Aliongeza kuwa Chama hicho kinashirikiana na Maafisa Ushirika kuendelea na maandalizi ya msimu katika kuangalia masuala ya usafirishaji wa malighafi kutoka kwa wakulima hadi kufikia maghalani hususani maeneo yenye changamoto za miundombinu.