************************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
29,sept
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Kibaha Vijijini ,Mkoa wa Pwani Michael Mwakamo, ameelezea kusikitishwa kwa kitendo cha wanafunzi wanaodaiwa hela ya chakula,kurudishwa nyumbani.
Aidha amewaasa, wazazi na walezi kutokukubaliana kwa baadhi ya mambo ambayo baadae yanakwenda kuwagharimu wenyewe, kwani makubaliano hayo mwisho wa siku yanakuwa sheria na kuwabana .
Mwakamo aliyasema hayo katika Vitongoji vya Kilangalanga, Janga na Mtongani akizungumza na wakazi kwenye mkutano wa Kampeni, ambapo alisema kurudishwa kwa wanafunzi kisa hela ya chakula binafsi kinamkera.
Akielezea mikakati ya kupambana na hilo, Mwakamo alisema muarubaini ni kujengwa sekondari maeneo ya karibu, hali itayowapatia fursa wanafunzi kuweza kukimbia nyumbani kula kisha kurejea shule, jambo ambalo Ilani ya CCM 2020/2025 imeliona hilo na kwenda kulifanyia kazi.
“Nitalifanyia kazi hili ,wanafunzi hawa ni watoto wetu wote ,inakera kuona wanafunzi wanarudi majumbani kisa chakula”;
“Ilani yetu iliyopitishwa na viongozi wetu ngazi za juu chini ya Jemedali wetu John Magufuli imesheheni mambo mbalimbali yanayokwenda kutekelezwa, ,” alieleza Mwakamo.
Nae mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Ludovic Remy aliwataka wana-Kibaha Vijijini kutorubunika kwa wagombea wanaotokea vyama vingine kwani ilani ya chama inatekelezwa.
“Tunawaona wanasiasa wenzetu wanakuja kunadi sera zao, tuwasikilize lakini mwisho wa siku tuwachague wanaotokea chama chetu,Rais, mbunge ,madiwani ambacho kina sera inayotekelezeka ukilinganisha na vyama vya wenzetu,” alisema Ludovick.