************************************
NA FARIDA SAIDY, MOROGORO.
Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amewataka watumishi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi ambao kwa kiasi kikubwa wanawahitaji watendaji hao.
Katibu Mkuu Kusaya ametoa wito huo leo (29.09.2020) Mkoani Morogoro wakati alipofungua mafunzo ya siku nne kwa wakuu wa Taasisi, Wakala na Bodi zilizo chini ya wizara ya kilimo kuhusu kamati za kudhibiti uadilifu wa watumishi wawapo kazini.
Aidha Kusaya amewataka watumishi wote kuwa waadilifu ndani na nje ya ofisi ili watende kazi kwa haki walizokabidhiwa kama dhamana ya kuhudumia watanzania bila upendeleo na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Hata hivyo amesema kuwa Wizara inatabumbua utendajikazi wa kila mtumishi ilie chini ya wizara hiyo,hivyo amewataka kutenda haki kwa wananchi pindi wawapo sehemu za kazi kwa kuepuka vitendo vinavyokiuka misingi ya maadili ikiwemo rushwa, kauli mbaya na matumizi mabaya ya madaraka.
Akitoa neno la Shukrani kwa Katibu wizara ya Kilimo Mkurugenzi Mkuu wa Wakala Udhibiti wa Viuatilifu (TPRI) Dkt. Magret Mollel amemshukuru Katibu Mkuu kwa kutoa kibali cha kufanyika mafunzo hayo yenye kulenga kuongeza tija na utendaji kazi wa wizara ya kilimo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Wizara ya Kilimo Filbert Lutare alisema mafunzo hayo yanahusisha washiriki 130 toka taasisi 23 chini ya wizara na kuwa wizara itahakikisha baada ya mafunzo haya watumishi kwenye taasisi zote wanaishi uadilifu na kuongeza kiwango cha maadili mema katika kuhudumia umma.
Mafunzo haya yanawakutanisha wakuu wa taasisi, bodi za mazao na wakala pamoja na kamati za uadilifu toka taasisi zote 23 chini ya wizara ya kilimo ambapo lengo ni kujifunza namna ya kuishi uadilifu katika kuhakikisha shughuli za serikali zinafikia malengo yaliyowekwa huku watumishi wakizingatia misingi ya uadilifu na maadili .