**************************************
NA SULEIMAN MSUYA
KATIKA kuhakikisha nchi ya Tanzania haingii katika mtego wa matumizi ya bidhaa zinazotokana Teknolojia ya Uhandisi Jeni (GMO) wanadau wameshauri kuwepo na mjadala wa kitaifa na kutolewa elimu kuanzia shule ya msingi kuhusu madhara yake.
Wadau hao wanakuja na ushauri huo ambapo kwa sasa dunia nzima pamoja na kuwepo mikataba, sheria, kanuni na miongozo ya uzalishaji na matumizi ya bidhaa hizo wanapiga vita kwa kile kinachodaiwa bidhaa za GMO kuwa na madhara kwa viumbe hai.
Wakichangia kwenye warsha ya siku moja iliyofanyika jijini Dar es Salaam na kushirikisha wakulima wa kilimo hai na wanaharakati wanaopambana na matumizi ya GMO wadau hao walisema mapambano dhidi ya bidhaa hizo yanahitaji elimu na mjadala wa kitaifa.
Abdallah Mkindi kutoka Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO), alisema kuruhusu GMO nchini ni kurudisha nyuma mkulima kwa kuwa mbegu hizo sio endelevu.
Alisema wanatarajia mwishoni mwa mwaka huu jijini Dodoma wataandaa tukio ambalo litajikita kwenye kuzungumzia chakula na mbegu ili kusaidia jamii kuelewa kwa kina madhara ya GMO.
Mkindi alisema TABIO imekuwa ikishirikiana na mashirika ya ndani na nje kuhakikisha wakulima wanazingatia kilimo hai ambacho kinatumia mbegu asili na kuachana na mbegu ambazo sio za kudumu.
“Sisi TABIO tumedhamiria kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha GMO haingii nchini kwa njia yoyote kwani ushahidi upo kuwa bidhaa na mbegu zake zina madhara kwa binadamu na viumbe hai wengine,” alisema.
Alisema hoja ya watu wa GMO imejikita katika ukame, wadudu vamizi na mabadiliko ya tabia nchi hali ambayo inaweza kudhibitiwa kwa kuwepo elimu ya kutunza mbegu asili kama ilivyokuwa zamani na kuhamasisha utunzaji mazingira.
Mwakilishi kutoka Kundi la Kupinga Matumizi ya GMO Tanzania, Albert Kamala alisema iwapo hakutakuwa na kauli moja baina yao kuna dalili ya jamii kuangamia siku chache zijazo.
Kamala alisema wao wameamua kupinga GMO kwa kuwa wanajua na kuona madhara yake kuanzia shambani hadi majumbani hivyo wanaamini Serikali inapaswa kuunga mkono kwa nguvu zote ili utekelezaji uonekane.
“Tumeamua kuwakutanisha hapa leo ili tuweze kuzungumza lugha moja kati ya sisi wanaharakati wa kupinga GMO na wakulima na baadae tupeleke ujumbe mmoja Serikalini ili hatua zichukuliwe kwani dalili sio nzuri iwapo tutaruhusu kilimo na matumizi ya bidhaa hizo katika nchi,” alisema.
Naye Sabrina Masinjila alisema utafiti unaonesha kuwa mbegu za GMO zimeendelea kuwa na athari zaidi kuliko faida kwa wakulima hivyo zinapaswa kupingwa kila mahali.
“Inasemekana mbegu hizo zinaimarisha wadudu vamizi, lakini kilimo hicho kinataka nafasi sana jambo ambalo ni changamoto kwa wakulima wadogo hata huko katika nchi ambazo zilianza zimeanza kuacha kwani hasara ni kubwa zaidi,” alisema.
Aidha, alisema taarifa mbalimbali zinaonesha kuwa mazao yatokanayo na GMO yamekuwa yakichangia ongezeko la saratani duniani hivyo hakuna sababu ya kuunga mkono.
Masanjila alisema Tanzania inapaswa kuwa na mjadala wa kitaifa ambao utatoa muongozo wa nini cha kufanyika ili kutoka katika janga hilo.
Bonaventure Charles Mwanharakati wa kupinga GMO kutoka Arusha aliomba Watanzania wapaze sauti ili kuhakikisha mbegu NA bidhaa za GMO hazipati nafasi nchini.
Mwanaharakati huyo alisema juhudi zielekezwe kwenye matumizi ya mbegu asili ambazo zinaonesha kuwa na matokeo chanya kwa miaka mingi.
“Pamoja na kupaza sauti pia kuwepo mashamba darasa ambayo yatasaidia wakulima kutambua mbegu asili ni zipi na GMO ni zipi kwani wakati mwingine ni changamoto kutambua,” alisema.
Ofisa Miradi wa Umoja wa Walima Matunda na MbogaMboga Zanzibar (UWAMWIMA) Khamis Issa Mohammed, alisema mjadala wa kitaifa utasaidia jamii kutambua thamani ya chakula na mbegu asili kwenye maisha yao tofauti na ilivyo sasa.
Mohammed alisema ufanisi wa mjadala huo unatakiwa kuhusisha makundi yote muhimu ambao ni wakulima, wanaharakati, waandishi wa habari, wanadau wa maendeleo na Serikali ili kuwa na mtazamo mmoja.
Mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi Mkoani Dar es Salaam (DCPC), Irene Mark alisema mapambano ya GMO yanaweza kufanikiwa iwapo elimu itatolewa kuanzia elimu ya msingi.
Aidha aliwataka wadau kuwatumia waandishi wa habari kuanzia ngazi za awali katika mapambano hayo na sio kusubiri kuwapa taarifa ya utekelezaji.
“Mimi naamini mapambano haya yanahitaji kujikita kuanzia elimu ya msingi, ila naomba msitutumie kuripoti mliochokiona tuwekeni kwenye mipango yenu kuanzia ngazi ya awali tutafika pamoja,” alisema.
Kwa upande wake Mtafiti wa Kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI -Dakawa), John Joseph alisema changamoto ya GMO inahitaji uwanda mpana wa mjadala ili kuwa kitu kimoja.
Alisema TARI-Dakawa wanaendelea na utafiti wa mbogamboga asili hivyo ni imani yake suluhu ya mbegu zenye mashaka itapatikana.
Akiwasilisha mada katika warsha hiyo ya siku moja Mwanasheria kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Isakwisa Mwamukonda alitoa rai kwa wanaharakati wanaopinga GMO kufanya utafiti wa kina kuhusu mbegu na bidhaa kwa kuwa ina faida na hasara.
Mwamukonda alisema iwapo bidhaa na mbegu GMO zipo nchini ni wazi kuwa zipo kisheria kwa kuwa sheria zetu zinaruhusu ila kwa kufuatwa hatua mbalimbali muhimu.
“Tanzania imesaini mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa Bioaniwai (1992), Mkataba Mdogo wa Cartagana (2002), Mkataba wa Nagaya.
Sera ya Taifa Mazingira (1997), Sera ya Taifa ya Biotechnolojia ya Kisasa (2009), Sera ya Kilimo ya (2019), Sheria ya Mazingira ya (2004) na Sheria za Kisekta,” alisema.
Mwanasheria huyo alisema katika kukabiliana na GMO nchini ni lazima wafanye utafiti wa kina ambao utawezesha watunga sera kuelewa na kufanya maamuzi sahihi.
Mmoja wa Waandaaji wa warsha hiyo, Austin Makani alisema warsha hiyo imewapa muongozo wa nini cha kupeleka Serikalini ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya hofu ya bidhaa na mbegu za GMO nchini.
“Kwa ujumla tunashukuru na tumepokea michango yote ambayo imetolewa na tutahakikisha inafika sehemu husika kwa hatua zaidi,” alisema.