Home Mchanganyiko DC MAGU AAHIDI PIKIPIKI YA WAGONJWA KISIWA CHA IJINGA

DC MAGU AAHIDI PIKIPIKI YA WAGONJWA KISIWA CHA IJINGA

0

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli,akipanda mtumbwi kuelekea katika Kisiwa cha Ijinga wilayani humo kwa ajili ya kuangalia changamoto za wananchi wa kisiwa hicho na kuzitatua.

Wananchi wa kisiwa cha Ijinga wamkisikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo  Salum Kalli (kulia) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye shule ya msingi Ijinga jana.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ijinga kisiwani Amos Vegule (kushoto) akitoa taarifa ya utendaji na utoaji huduma kwa wananchi lakini pia changamoto za zahanati hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Magu , Salum Kalli (kulia) jana.Picha Zote na Baltazar Mashaka

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli akitembea kwenda nchi kavu baada ya kushuka kwenye mtumbwi alipofanya ziara ya kutembelea kisiwa cha Ijinga wilayani humo jana akiwa Mkuu wa Wilaya wa pili kutembelea kisiwa hicho tangu nchi kupata uhuru.

**************************************

NA BALTAZAR MASHAKA, Magu

MKUU wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, ameahidi kutafuta pikipiki ya miguu mitatu (ambulance) ya kubeba wagonjwa katika Zahanati ya Kijiji cha Kisiwa cha Ijinga wilayani humo.

Alitoa ahadi hiyo jana alipozungumza na uongozi wa zahanati hiyo pamoja na  wananchi wa kisiwa hicho kilichopo ndani ya Ziwa Victoria, wilayani Magu mkoani Mwanza baada ya kuzuru kisiwani hapo kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo Julai 3, mwaka huu.

Alisema kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kutafuta pikipiki ya kubeba wagonjwa hasa wajawazito wanaohitaji huduma za dharura za kujifungua na wagonjwa mahututi wenye rufaa za kwenda Hospitali ya Wilaya ya Magu ama Kituo cha Afya Kahangara.

Awali Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo  Amos Vegule, alisema wana tatizo la usafiri kwa wagonjwa wa rufaa na huduma ya dharura ya uzazi hivyo wanahitaji pikipiki ili kukabili changamoto hiyo.

Pia alieleza kuwa  zanahati hiyo ina changamoto ya ukosefu wa majengo ya wagonjwa wa nje na maabara pamoja na uhaba wa nyumba za watumishi kati ya watano waliopo ambapo wawili wameoa na wana familia.

“Zahanati ina dawa za kutosha an inatoa huduma nzuri kwa jamii lakini ipo changamoto ya uhaba wa nyumba za watumishi, jengo la maabara na la wagonjwa wa nje, tunahitaji mashine tarakakishi (kompyuta) ya kutunza kumbukumbu lakini nishati ya umeme wa mfumo jua iliyopo haitoshi, hivyo tunatakiwa kupata umeme wa gridi hapa kisiwani,” alisema Vegule.  

Aidha wananchi wa kisiwa hicho waliomba mkunga muuguzi mmoja wa kuwahudumia akina mama wanaojifungua kwa madai kuwa zahanati hiyo ina watumishi wa kiume tu ambao kwa namna moja ama nyingine inawawia vigumu wananwake kujieleza  kwa uwazi wanapokwenda kupata huduma