Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli,akipanda mtumbwi kuelekea katika Kisiwa cha Ijinga wilayani humo kwa ajili ya kuangalia changamoto za wananchi wa kisiwa hicho na kuzitatua.
Wananchi wa kisiwa cha Ijinga wamkisikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Salum Kalli (kulia) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye shule ya msingi Ijinga jana.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ijinga kisiwani Amos Vegule (kushoto) akitoa taarifa ya utendaji na utoaji huduma kwa wananchi lakini pia changamoto za zahanati hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Magu , Salum Kalli (kulia) jana.Picha Zote na Baltazar Mashaka
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli akitembea kwenda nchi kavu baada ya kushuka kwenye mtumbwi alipofanya ziara ya kutembelea kisiwa cha Ijinga wilayani humo jana akiwa Mkuu wa Wilaya wa pili kutembelea kisiwa hicho tangu nchi kupata uhuru.
**************************************
NA BALTAZAR MASHAKA, Magu
MKUU wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, ameahidi kutafuta pikipiki ya miguu mitatu (ambulance) ya kubeba wagonjwa katika Zahanati ya Kijiji cha Kisiwa cha Ijinga wilayani humo.
Alitoa ahadi hiyo jana alipozungumza na uongozi wa zahanati hiyo pamoja na wananchi wa kisiwa hicho kilichopo ndani ya Ziwa Victoria, wilayani Magu mkoani Mwanza baada ya kuzuru kisiwani hapo kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo Julai 3, mwaka huu.
Awali Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo Amos Vegule, alisema wana tatizo la usafiri kwa wagonjwa wa rufaa na huduma ya dharura ya uzazi hivyo wanahitaji pikipiki ili kukabili changamoto hiyo.
Pia alieleza kuwa zanahati hiyo ina changamoto ya ukosefu wa majengo ya wagonjwa wa nje na maabara pamoja na uhaba wa nyumba za watumishi kati ya watano waliopo ambapo wawili wameoa na wana familia.
“Zahanati ina dawa za kutosha an inatoa huduma nzuri kwa jamii lakini ipo changamoto ya uhaba wa nyumba za watumishi, jengo la maabara na la wagonjwa wa nje, tunahitaji mashine tarakakishi (kompyuta) ya kutunza kumbukumbu lakini nishati ya umeme wa mfumo jua iliyopo haitoshi, hivyo tunatakiwa kupata umeme wa gridi hapa kisiwani,” alisema Vegule.