Mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel akipata maelezo juu ya OSHA mara baada ya Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi Khadija Mwenda kumtembelea ofisi kwake, wakati wa Maonesho ya tatu ya teknolojia na uwekezaji kwenye sekta ya madini yanayofanyika mjini Geita.
Baadhi ya wananchi wakipata huduma ya upimaji wa macho kwenye banda la OSHA kwenye Maonesho ya tatu ya teknolojia ya uwekezaji kwenye sekta ya madini, kwenye viwanja vya Bombambili Mjini Geita
Waziri wa Madini Dotto Biteko akipata maelezo kwenye banda la OSHA kuhusu shughuli za OSHA mara baada ya kutembelea banda la OSHA kwenye Viwanja vya Bombambili mjini Geita, wakati wa maonesho ya tatu ya Teknolojia na uwekezaji kwenye sekta ya madini
kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi Khadija Mwenda akipata maelezo kutoka kwa moja ya washiriki wa Maonesho, wachimbaji wadogo kwenye Maonesho yanayoendelea ya tatu ya teknolojia ya uwekezaji kwenye Sekta ya madini Mjini GeitaMhandisi Maria Edward Ndaskoy akitoa maelezo juu ya usalama wa mifumo ya Umeme kwa wananchi waliotembelea banda la OSHA kwenye Maonesho ya tatu ya Teknolojia ya Uwekezaji kwenye sekta ya Madini, mjini Geita.
***************************************
Mwandishi wetu,Geita
Serikali imeuagiza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuandaa na kutekeleza programu maalum ya mafunzo ya Usalama na Afya kwa wachimbaji wadogo katika mikoa yote nchini yenye shughuli za uchimbaji madini ili kupunguza ajali na magonjwa yatokanayo na kazi katika sekta hiyo muhimu katika uchumi wa nchi.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Madini, Doto Biteko, alipotembelea banda la OSHA katika maonesho ya Tatu ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani Geita.
Waziri Biteko ameeleza kuridhishwa kwake na mafunzo ya usalama na afya kazini ambayo yamekuwa yakitolewa na OSHA kwa baadhi ya makundi ya wachimbaji wadogo na kuahidi kuwapa ushirikiano OSHA kupitia Wizara yake.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel, amewataka wadau wa sekta ya madini na sekta nyingine za kiuchumi katika mkoa wake kuzingatia misingi ya usalama na afya katika shughuli zao za uzalishaji.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema baada ya maonesho hayo taasisi yake itaandaa mpango mahsusi wa kutoa mafunzo hayo ya usalama na afya kwa wachimbaji wadogo katika mikoa yote yenye shughuli za uchimbaji madini.
Baadhi ya wadau waliotembelea maonesho akiwemo………….wameeleza kufurahishwa kwao na mafunzo ambayo wameyapata kutoka OSHA wakati wa maonesho hayo ya Tatu ya Teknolojia ya Madini.
OSHA ni taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu yenye wajibu wa kulinda nguvukazi ya nchi kupitia kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.