Kaimu Mkurugenzi kutoka Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Maji Bw. Teddy Mwaijumba kushoto kwake akiwa na Meneja wa RUWASA katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Mhandisi Mapambano Boniface wakikagua miundombinu ya mradi wa maji wa dharula wa Kaliua katika kijiji cha Kazana Upate.
Kaimu Mkurugenzi kutoka Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Maji Bw. Teddy Mwaijumba akiwa na Meneja wa RUWASA Mkoa Mhandisi Lameck Kapufi, Meneja wa RUWASA Halmashauri ya Kaliua Mhandisi Mapambano Boniface na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaliua Bw. Michael Nyainda wakijadili jambo baada ya kukagua mradi wa maji wa dharula wa Kaliua mjini katika kijiji cha Kazana Upate.
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Bw. Abel Busalama akiwa na Timu ya Viongozi na Watalaam kutoka Wizara ya Maji, RUWASA mkoa wa Tabora na RUWASA Wilaya ya Kaliua wakijadili jambo mara baada ya kukagua miundombinu ya mradi wa maji katika kijiji cha Kazana Upate.
Mwananchi katika kijiji cha Ideka Bi. Tausi Haruna Said akipata huduma ya majisafi na salama karibu na makazi yake mara baada ya upanuzi wa mradi wa maji kutoka kijiji cha Mabama kuja Ideka kukamilika mwezi Machi, 2020, wananchi wa kijiji hiki hawajawahi kupata majisafi na salama tangu nchi yetu kupata uhuru mwaka 1961.
…………………………………………………………….
Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika mji wa Kaliua imeboreka baada ya Serikali kutekeleza mradi wa maji wa dharura ulioinua kiwango cha upatikanaji maji kutoka hali ya kutokuwa na huduma ya uhakika ya maji hadi kufika asilimia 44. Mradi huo wa dharura ulikamilika mapema mwezi Februari 2020.
Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Kaliua Mhandisi Mapambano Boniface amesema kazi ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji inaendelea vizuri na umakini wa hali ya juu unatumika katika kutafuta maji chini ya ardhi ili kujiridhisha na kiwango na ubora wa maji.
“Miradi inatekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Maji wa Taifa, Programu za Payment by Results (PbR) na Payment for Results (PfR)” , Mhandisi Mapamabano amesema na kuongeza lengo walilojiwekea ni kufikia malengo makubwa zaidi kwa wananchi kupata maji bombani.
Pamoja na hayo, Meneja wa RUWASA katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mhandisi Godfrey Shibiti amesema kupitia Programu ya Payment by Results (PbR) Serikali imekamilisha upanuzi wa mtandao wa maji wa kilomita 5.3 kutoka katika kijiji cha Mabama hadi kijiji cha Ideka ambapo wananchi wanapata huduma ya maji tangu Mwezi Machi, 2020.
Kazi hiyo ya kuwafikishia wananchi huduma ya maji imefanywa kwa ushirikiano wa watendaji wa Wizara ya Maji kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA), Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika.
Kufuatia ubunifu huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Mipango, Wizara ya Maji Bw. Teddy Mwaijumba amewapongeza watendaji hao wa sekta ya maji na kuwataka kuimarisha ushirikiano zaidi katika kutekeleza miradi ya maji na utunzaji wa vyanzo vya maji katika mkoa wa Tabora.
Aidha, Bw. Teddy amewataka TUWASA kuongeza mtandao wa mradi wa maji kutoka ziwa Victoria ili kumaliza kabisa tatizo la maji katika baadhi ya maeneo yenye upungufu wa huduma hiyo muhimu.
Mradi wa maji wa dharura wa mjini Kaliua umetekelezwa kupitia Mkandarasi kampuni ya Monimar & Sons Co Ltd na Serikali imelipa kiasi cha shilingi milioni 571.6, ambapo wananchi zaidi ya elfu 17 hivi sasa wanafaidika na huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza.