WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika kongamano la Amani lililoandaliwa na Baraza la Vijana Zanzibar katika ukumbi wa Baraza la Sheikh Idrissa Abdul Wakil.
………………………………………………………………
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Hussein Ali Mwinyi amewasihi vijana kuwaepuka wanasiasa wenye Sera za kuingiza nchi katika vurugu na machafuko.
Amesema wanasiasa wanaofanya siasa za uchochezi hawafai kuaminiwa na kupewa nafasi yoyote ya uongozi kwani matendo yao yanaenda kinyume na Katiba,miongozo na utamaduni wa Kitanzania.
Alisema kuwa vijana wengi wamekuwa wakitumiwa kuvunja amani ya nchi jambo ambalo ni hatari kwa maendeo ya taifa na ustawi wa jamii,hivyo kundi hilo la vijana wanatakiwa kuepuka kutumiwa kuvunja amani kwa maslahi ya watu wachache.
Alieleza kuwa mara nyinyi uvunjifu wa amani hauletwi na wazee wala watoto bali chanzo chake ni vijana kutokana na kutumiwa na watu ambao hawana nia njema na nchi yao.
Kauli hiyo alilitoa katika kongamano la siku ya amani duniani lilofanyika katika ukumbi wa Shekh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.
Alisema, watu wengi hudhani amani inaletwa na vyombo vya ulinzi na usalama sivyo ilivyo bali amani huletwa na utulivu wa wananchi na kupata maendeleo.
“Sio idadi ya askari tulionao, ubora wa zana za kijeshi tulizonazo zinazoweza kuleta amani bali amani huletwa na utulivu wa wananchi na Tanznaia tunajivunia kuwa na wananchi wapenda amani,” alisema.
Dk. Mwinyi ambae pia ni mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi alibainisha kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kwamba amani tuliyonayo inaendelea kudumu milele.
Alifahamisha kuwa zipo nchi ambazo zimeichezea amani ya nchi zao duniani na kupelekea machafuko ikiwemo Siriya,Yemen, Iraq, Kongo na nchi nyengine.
“Nchi hizi ziwe fundisho tosha kwetu kuona athari za kuivuruga amani ni hatari kubwa hasa kwa wanawake na watoto Tanzania tunahitaji amani katika kuwaletea maendeleo wananchi wetu hivyo sisi tuwe ni sehemu ya kuijenga na kuiendeleza amani yetu,” alisisitiza.
Hivyo, alisisitiza kuwa wananchi wana kila sababu ya kudumisha amani iliyopo na kuwa mabalozi wa amani katika nchi yao ili kuendelea kupata maendeleo maendeleo.
Sambamba na hayo alisema vijana ndio wadau wakubwa wa amani hivyo ni lazima kutumia nafasi hiyo katika kulaani vitendo vya uvunjifu wa amani popote pale inapotokea.
Mbali na hayo Dk. Mwinyi aliwataka vijana kutumia siku hiyo kuwa chachu ya vijana na ari mpya kuhakikisha wanailinda amani iliyopo nchini kwa nguvu zao zote.
Alitumia muda huo kuipongeza serikali ya awamu ya saba kwa hatua ya kuanzisha kwa Baraza la vijana Zanzibar ambalo linajenga taifa la baadae litakalotetea nchi yao.
Hivyo, aliwasisitiza viongozi wa baraza hilo kuendelea kujenga umoja wao ili kutoa fursa kwa serikali katika kuwasaidia vijana katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumzia malengo yake kwa serikali ya awamu ya nane aliwataka vijana kuendelea kuwa na matarajio kwake katika kujenga uchumi mpya wa Zanzibar kupitia utalii, mafuta na gesi na Viwanda.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Khamis Faraj Abdalla, akitoa salam za vijana alisema siku hiyo ina lengo la kuimarisha umoja na mshikamano wa taifa lao sambamba na kuwapa elimu ya uzalndo katika kulinda amani ya nchi wakati wote.
Alipongeza SMZ na SMT katika kusimamia suala la amani katika kipindi chote kuona Tanzania inaendelea kuwa salama.
Akizungumzia lengo la kuunda mabara ya vijana alisema ni kuwaunganisha vijana pamoja na kuwajenga kuwa wazalendo katika kuitetea nchi yao.
Aidha alisema serikali ya CCM inatekeleza ilani kwa vitendo katika kuwajali vijana na kuwawezesha kwa kuwapa mikopo ambayo inawawezesha kujiajiri kupitia kazi za mikono.
Hivyo aliwasisitiza vijana kushirikiana na CCM katika kuisimamia amani kwa kipindi chote cha uschaguzi na kutambua kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi.
Nao vijana kutoka vyuo vikuu na mabaraza ya vijana Zanzibar, walimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika kusimamia suala la amani ya nchi na kuahidi kuilinda na kuitetea wakati wote ili iendelee kudumu.
Katika kongamano hilo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo wajibu wa jamii katika kulinda amani ya nchi, umuhimu wa kutoa taarifa za uvunjifu wa amani ambapo kauli mbiu ni “Tudumishe amani kwa pamoja”.