*****************************
NA EMMANUEL MBATILO
Wazazi, walezi na familia wahimizwa kuwapeleka watoto wanaostahili kupata chanjo vituoni ili wapate chanjo stahiki kwa ratiba iliyopangwa.
Ameyasema hayo leo Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt.Ayoub Kibao katika Semina ya Wanahabari Kuhusu Chanjo iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akifungua semina hiyo Dkt.Kibao amesema kila mmoja wetu anawajibu kuhakikisha mtoto wake, mtoto wa jirani au mtoto yeyote yule anapewa haki ya kupata chanjo ili asiwe hatari kwa wengine kwa kusababisha milipuko ya magojwa.
“Bado kumekuwa na idadi ya watoto wasiokamilisha chanjo na wasiochanjwa kwenye baadhi ya maeneo na hivyo kusababisha uwezekano wa milipuko ya Surua”. Amesema Dkt.Kibao.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na shirika la Gavi, na wadau wengine wa Maendeleo, imefanikiwa kununua jumla ya magari 74 kuimarisha huduma za chanjo hapa nchini.
“Serikali ya awamu ya 5 imedhamiria kuwa kila Halmashauri hapa nchini inakuwa na gari la kusambaza chanjo. Kwa kipindi cha 2012 hadi 2015 jumla ya halmashauri 78 zilipatiwa magari ya kusambazia chanjo, na mwaka 2019 Serikali ilitoa magari 61 katika halmashauri nyingine. Na mpaka kufikia mwaka 2021/2022, halmashauri zote zilizobaki nchini zitakuwa zimepatiwa magari ya chanjo”. Amesema Dkt.Kibao.
Kwa upande wake Afisa Mradi Mpango wa Taifa wa Chanjo Wizara ya Afya Bi.Lotalis Gadau amesema watu wasiopata chanjo wana nafasi ya kubwa zaidi kupata maambukizi ya magonjwa kulingana na wale waliopata chanjo.
“Magonjwa yanayozuilika kwa chanjo yanasambaa kwa kasi kwenye jamii ambayo ina watu ambao hawajapata chanjo, wakina mama pamoja na kusadiwa na wakina baba wanatakiwa kuwapeleka watoto wao waweze kupata chanjo ili kuepuka kwa kiasi kikubwa magonjwa ambayo yanazuilika kwa chanjo”. Amesema Bi, Lotalis.
Pamoja na hayo amesema miongoni mwa malengo ya mpango wa taifa wa chanjo ni pamoja na kupumguza magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kwa uanzishaji chanjo mpya ambazo hazitolewi kwa sasa.
Hata hivyo amesema msichana wa umri wa miaka 14 lazima akamilishe dozi mbili za chanjo ya HPV, dozi ya pili miezi 6 baada ya kupata dozi ya kwanza.