Mtafiti Mwandamizi na Mdhibiti wa Visumbufu vya Wadudu na Magonjwa kwenye zao la korosho, kutoka Tari- Naliendele Mtwara, Dkt.Wilson Nene, akiwaeleza Maafisa Ugani na Wakulima namna ugonjwa wa Ubwiriunga unavyoathiri mikorosho wakati wa mafunzo kwa vitendo yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Mnyakongo wilayani Kongwa mkoani Dodoma jana..
Mtafiti wa Kilimo kutoka Tari Naliendele, Selemani Libaburu, akionesha namna ya kutumia mashine ya kupulizia (Motorized Blower).
Na Godwin
Myovela, Kongwa Dodoma
KITUO cha
Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele hatimaye kimetoa majawabu ya namna ya
kudhibiti visumbufu vya wadudu waharibifu na magonjwa, ikiwemo ugonjwa wa
Ubwiriunga, ugonjwa wa Blaiti na Debeki ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa ni
changamoto kwa ustawi wa zao la korosho ndani ya Wilaya ya Kongwa na kwingineko
nchini
Athari
nyingine zilizoonekana wazi ndani ya wilaya hiyo na kupatiwa ufumbuzi na Tari
Naliendele ni pamoja na kukithiri kwa wadudu waharibifu wa zao hilo wakiwemo
Mbu wa Mikorosho, Mbu wa Minazi na Vidung’ata ambao ni kikwazo kikubwa cha
ukuaji mzuri wa zao la Korosho ambalo linatajwa kuwa ni zao lenye uchumi mkubwa
na soko la uhakika
Akizungumza
kwenye mafunzo ya Kilimo Bora cha Korosho yaliyotolewa jana wilayani hapa kwa
wakulima na Maafisa Ugani, Mtafiti kutoka TARI Naliendele Programu ya Korosho,
Kitengo cha Udhibiti wa Visumbufu vya Wadudu waharibifu na Magonjwa, Dk Wilson
Nene, alisema ugonjwa wa ubwiriunga kama usipodhibitiwa hugeuka tishio kwa ustawi wa mkorosho na hasara yake ni kuanzia asilimia 70
mpaka 100 (kwa maana ya kutoambulia mavuno yoyote)
“Hapa Kongwa
kwenye mashamba tuliyokwenda kufanyia ‘field’ tumeona kuna changamoto ya
magonjwa kwa mikorosho mingi kuwa na matatizo ya wadudu waharibifu hasa mbu wa
mikorosho, mbu wa minazi na ugonjwa wa ubwiriunga,” alisema Nene
Alisema
wadudu hao wakiwa wengi na kushambulia kwa kasi husababisha majani ya mkorosho
husika kuathirika, na zaidi majani yake hubadilika na kuonekana yameungua au
mfano wa kitu kilichoungua au kubabuliwa na moto au moshi
“Hali hiyo
hutokana na wadudu hawa waharibifu mbu wa minazi na mbu wa mikorosho wanapokuwa
wanafyonza kwenye majani ‘maeneo teketeke’…basi pale walipofyonza inatokea
vidonda ambapo ndio sehemu kimelea hicho kinachosababisha ugonjwa unaoitwa
‘Debeki’ kinapoingilia. Ndio maana hapa Kongwa tumekuta baadhi ya mikorosho
imeathiriwa na Debeki,” alisema
Dk Nene
alisema kuna umuhimu mkubwa kwa wakulima wa Kongwa, na wengine waliopo mikoa
yote 17 inayolima zao hilo nchini kwanza kutambua wadudu waharibifu na magonjwa
ya mkorosho kabla athari hazijajitokeza lakini pia kuzingatia mafunzo ya namna
ya kudhibiti kitaalamu yanayoendelea kutolewa na TARI kwa sasa
Alieleza
kwamba kuna njia kuu tatu za kudhibiti ambazo ni njia za asili kwa maana ya
usafi shambani, kuanzia katika upandaji-kupanda kwa nafasi, lakini pia
mikorosho yako isisongamane ili kuweza kupogolea. Kwa kufanya hivyo mkulima
atatengeneza mazingira yasiyo-rafiki kwa vimelea na wadudu hao waharibifu
Aidha, njia
nyingine ni matumizi ya aina 54 ya mbegu bora zinazozalishwa na kituo cha
utafiti wa kilimo Tari Naliendele, na kwa kufanya hivyo shamba la mkulima
litakuwa na tija na ubora sambamba kuongezeka kwa kiwango cha uzalishaji bila
kusahau matumizi sahihi ya viuatilifu na aina zake zote sanjari na matumizi
bora ya mashine za kupulizia
“Kupitia
elimu hii ambayo imekuwa na mwamko mkubwa tunaamini wilaya ya Kongwa na
wakulima wengine za zao hili nchini sasa tutakwenda kuleta mchango mkubwa kwa
kuongeza uzalishaji mara 4 kutoka kiwango cha sasa cha tani laki 3.15 kufikia
tani milioni 1 kama shabaha ya taifa kufikia 2023.