Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Prof.Ibrahim Juma akioneshwa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Mkalama litakaloanza kujengwa kabla ya mwisho ya mwaka huu.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Prof.Ibrahim Juma akimkabidhi machapisho ya Mahakama Mkuu ya wilaya ya Mkalama Mhandisi Masaka alipomtembelea ofisini kwake wakati wa ziara ya mkoani Singida.
…………………………………………………………………..
Na Lydia Churi -Mahakama Singida
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameishauri serikali kupanga bajeti kwa ajili ya uanzishwaji wa Mahakama pale inapoanzisha maeneo mapya ya utawala kama mikoa na wilaya ili kuwasogezea wananchi huduma ya Mahakama ambayo ni muhimu katika jamii.
Akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Mkalama, viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Iramba mkoani Singida pamoja na watumishi wa Mahakama katika ziara yake, Jaji Mkuu amesema Mahakama imekuwa nyuma kutokana na kusahaulika kupangiwa bajeti wakati yanapoanzishwa maeneo mapya ya utawala.
“Uamuzi unapofanywa wa kuanzisha mkoa au wilaya mpya, bajeti ya Serikali hupangwa ya kutosha kujenga vituo vya Polisi, Magereza na nyumba za watumishi na kusahau Mahakama ambayo ni huduma muhimu kwa wananchi”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema ujenzi wa majengo ya Mahakama ni muhimu kwa kuwa kutokuwepo kwa Mahakama huwanyima wananchi nafasi ya kudai haki kwani haki hiyo huweza kuchukuliwa na watu wengine wenye nguvu. Akitolea mfano kwa wajane, Jaji Mkuu amesema kutokuwepo kwa Mahakama ya Mwanzo katika eneo husika huwanyima wajane haki ya kwenda kudai mirathi yao.
“Ujenzi wa majengo ya Mahakama ni muhimu kwa kuwa unapeleka haki karibu zaidi na wananchi na kuwapa nguvu wanyonge ambao hawana uwezo wa haki yao”, alisisitiza.
Alisema Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano inakusudia kuanza ujenzi wa majengo ya Mahakama za wilaya katika wilaya 33 nchini ifikapo mwishoni mwa mwaka huu ili kusogeza huduma za Mahakama kwa wananchi na kuhakikisha haki inapatikana kwa wote na kwa wakati.
Kuhusu Ushirikiano wa Mihimili ya Dola, Jaji Mkuu amesema Mihimili yote inaunganishwa na wananchi kwani yote hufanya kazi zake kwa ustawi wa wananchi. Alisema matakwa ya wananchi yanailazimisha mihimili yote kushirikiana na pia Katiba ya nchi imegawa mamlaka kwa kila mhimili.
Wakati huo huo, Jaji Mkuu amewataka wapelelezi na waendesha Mashtaka nchini kujipanga vizuri katika ukusanyaji na upangaji wa ushahidi ili kurahisisha suala zima la upatikanaji wa haki.
“Mara nyingi shauri lisipoenda vizuri lawama huenda kwa Majaji na Mahakimu. Majaji na Mahakimu huongozwa na ushahidi uliowasilishwa au kutolewa mahakamani hivyo hawana budi kuwabana wapelelezi ili shauri likamilike kwa haki”, alisema Prof. Juma.
Aidha, aliwashauri wapelelezi na Waendesha Mashtaka kujenga utamaduni wa kusoma hukumu za Mahakama ya Rufani pamoja na zile za Mahakama Kuu kwa kuwa zinatoa mafunzo na kuonyesha ni mambo gani yafanyike ili mhalifu atiwe hatiani na asiye na kosa aachiwe huru kwa wepesi zaidi.
Jaji Mkuu anaendelea na ziara ya kikazi katika mkoa wa Singida ambapo tayari amekagua shughuli za Mahakama katika wilaya za Manyoni, Ikungi, Iramba na Mkalama.