Katibu Mkuu Wizara Madini Prof. Simon Msanjila akisaini Kitabu katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Rashidi Mwaimu.
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akieleza jambo kwenye Mkutano uliofanyka katika Soko la Madini ya Bati la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera. |
Baadhi ya washiriki walioshiriki Mkutano wa Katibu Mkuu Wizara Madini Prof. Simon Msanjila katika Soko la Madini ya Bati la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera. |
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila akiwa kwenye picha ya
pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali katika Soko la Madini ya Bati
la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera.
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof.Simon Msanjila ameshuhudia
biashara ya Madini ya Bati (Tin) ikifanyika ambapo Shirika la Taifa la
Uchimbaji Madini (STAMICO) likifanya manunuzi Kilo 2,271 ya Madini ya
Bati yenye thamani ya shilingi Milioni 34 kutoka kwa Wachimbaji Wadogo.
Katika ziara yake hiyo, Prof. Msanjila alitembelea Soko la
Madini la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera na kuzungumza na Wachimbaji
Wadogo pamoja na Wafanyabiashara wa Madini hayo.
Aidha Prof. Msanjila amewataka wachimbaji Wadogo na
Wafanyabiashara wa Madini ya Tin kulitumia Soko la Kyerwa kuuzia Madini
yao ili wanapotaka mkopo kutoka benki inakuwa rahisi kwa Wizara
kudhibitisha mauzo yao kwa kuwa yatatambuliwa kwenye mfumo wa Wizara.
Pia Prof. Msanjila amewasihi Wachimbaji Wadogo na
wafanyabishara wa Madini ya Bati kufungamanisha biashara ya madini na
chumi zingine kama kilimo, ufugaji n.k. ili kujiongezea wigo wa fursa
zitokanazo na Sekta ya Madini.
Katika ziara hiyo yenye lengo la kuhakikisha Soko la Madini
ya Bati la Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera limeanza kufanya kazi, Prof.
Msanjila aliambatana na viongozi Mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa
Wilaya ya Kyerwa Rashidi Mwaimu.
Vile vile, Prof. Msanjila amewasisitiza wachimbaji Wadogo
na Wafanyabiashara wa Madini ya Bati kuongeza juhudi za uzalisha wa
madini hayo kwani Soko la uhakika kwa sasa linapatikana na kuwataka
kuepuka utoroshaji wa madini hayo.
Pia, Prof. Msanjila maipongeza Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya Wilaya ya Kyerwa kwa ushirikiano na uzalendo waliouonesha katika
kulinda Rasilimali Madini kwa manufaa ya Nchi.
“Mwaka jana mwezi wa pili Tanzania tulifanikiwa kupata
Cheti cha Uhalisia wa Madini ya Bati ambapo Waziri Mkuu Kassim Mjaliwa
alikizindua cheti hicho hivyo, tuongeze juhudi kuzalisha Madini kwa
wingi na kuyaongezea thamani na hatimaye tuyapeleke nje ya nchi
tukawauzie”, alisema Prof Msanjila.
Wakati huo huo, Prof Msanjila alisikiliza kero na
changamoto za Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Bati pamoja na
Wafanyabiashara wa madini hayo na kuyatolea majibu papo hapo.
Pamoja na mambo mengine Prof. Msanjila alitembelea Viwanda
vya kuchakata Madini ya Bati kikiwemo Kiwanda cha African Top Mineral
Limited pamoja na Tanzplus ili kujionea shughuli za uongezaji thamani
katika viwanda hivyo zinavyo fanyika.
Prof. Msanjila amewataka wanunuzi wa Madini ya Bati
kuwalipa fedha zao Wachimbaji Wadogo kwa wakati na kuepuka usumbufu wa
kuwacheleweshea malipo yao.
Aidha, Prof. Msanjila amewataka Wachimbaji Wadogo na
Wafanyabiashara ya Madini ya Bati kupendana, kuthaminiana na kuachana na
mambo ya majungu ili waongeze tija kwenye shughuli yao ya uchimbaji
madini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Rashidi Mwaimu
alimpongeza Katibu Mkuu kwa ziara yake hiyo ambayo imesaidia kuondo
changamoto za Wachimbaji Wadogo na Wafanyabiasha wa Madini ya Bati
ambayo yalidumu kwa muda mrefu.