Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima (WAKWANZA KULIA) akizungumza na maafisa afya na timu ya Afya ya Halmashauri ya Chamwino iliopo mkoani Dodoma.
Wajumbe wa Timu ya Afya Halmashauri ya Chamwino wakimfatilia Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima (HAYUPO PICHANI) wakati alipofanya kikao na Timu ya Afya ya Halmashauri ya Chamwino mkoani Dodoma Wajumbe wa Timu ya Afya Halmashauri ya Chamwino wakimfatilia Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima (HAYUPO PICHANI) wakati alipofanya kikao na Timu ya Afya ya Halmashauri ya Chamwino mkoani Dodoma
………………………………………………………………………….
Na. Majid Abdulkarim, Chamwino.
Serikali imesema kuwa kila mjumbe wa Timu ya Afya Mkoa na Halmashauri anawajibu wa kujua na kuchangia mawazo juu ya uboreshaji katika kila kitengo kilichopo katika timu hiyo bila kujali kama ni eneo la taaluma yake tu bali kwa kuzingatia kwamba wao ni Timu.
Kauli hiyo imebainishwa jana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipofanya kikao na Timu ya Afya ya Halmashauri ya Chamwino mkoani Dodoma juu ya utekelezaji wa mpango maalumu wa usafi wa mazingira (Water, Sanitation and Hygiene) katika kata zao.
Aidha Dkt. Gwajima amezitaka Timu za Afya za Halmashauri nchini kubadilika katika mfumo wa uendeshaji wa vikao vyao vya utekelezaji wa majukumu kwa kila mjumbe kuwa wazi juu ya utekelezaji wa majukumu yake na wajumbe wengine kutamani kujua nini mwenzao anatekeleza na anachangiaje mafanikio au changamoto kwenye utekelezaji wa wengine.
Uendeshaji wa vikao ukiwa wa mwelekeo huu utaweza kuibua hoja chanya mbalimbali zenye umiliki wa wajumbe wote na hapo ndiyo kusudi la neno TIMU litatimia vizuri zaidi.
Vilevile Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa kila mjumbe wa timu ya afya mkoa na halmashauri akiwa na msingi wa uelewa juu ya majukumu ya mjumbe mwenzake itasaidia katika uboreshaji wa huduma katika idara husika kwa ladha ya kisekta kwani kila mjumbe atapata ushauri na kupewa mbinu mbali mbali za kuweza kufikia malengo tarajiwa ya idara husika na wajumbe wenzake.
“Uendeshaji wa vikao vyetu ukibadilika kwa kila mjumbe kushirikishwa kikamilifu kuliko mjumbe kushiriki yeye kama yeye ni matumaini yangu kuwa tutaweza fikia malengo kwa kasi zaidi kwani mtakuwa wengi na sio pekeyako katika kuhakikisha unapata matokeo ”, ameeleza Dkt. Gwajima.
Lakini pia Dkt. Gwajima ametoa rai kwa wataalamu wa afya nchini kuwa wahamasisha kwa kasi zaidi jamii kujenga vyoo bora na kulinda usafi wa mazingira katika kaya kwani kwa kufanya hivyo nchi inaweza kupunguza zaidi idadi ya wanaougua magonjwa yanazuilika.
Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima ametoa pongezi kwa Timu ya Afya Halmashauri ya Chamwino kwa kuitikia ushauri wake wa kuwataka kuchapa kazi na kuwa wabunifu na leo wamefanya vema katika kuongeza ushawishi kwa wananchi juu ya kujiunga na bima ya afya ya jamii iliyoboreshwa tofauti kabisa na mwaka uliopita.
“Mmenitia moyo na nimefarijika sana kuwa hakika ile ziara iliyotukutanisha na kujadili pamoja jinsi ya kufanya kazi kweli mlinielewa na leo nimeshudia matokeo yake”, amesisitza Dkt. Gwajima.
Hivyo Dkt. Gwajima amewataka watoe chapisho la mafanikio hayo kwenye jarda la halmashauri hiyo kwa kueleza hali ya awali ilikuwaje na sasa ikoje ndani ya mwaka mmoja tu ili kuhamasihsa wengine kuwa inawezekana ni jambo la kubadili mtazamo tu katika kufanya mambo.