Mgombea Urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania na mwenyekiti wa chama cha wananchi (CUF) Prof. Ibrahimu Haruna Lipumba akiwahutubia wananchi wa wilaya ya Kyerwa kwenye mkutano wa Kampeini mji mdogo wa Nkwenda Septemba 24,2020.
Wananchi wa mji mdogo wa Nkwenda wilayani Kyerwa wakimsikiliza na kumshangilia mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CUF Prof.Ibrahimu Lipumba kwenye mkutano wa kampeni.
*************************************
Na Allawi Kaboyo Kyerwa.
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi chama cha wananchi (CUF) na mwenyekiti wa chama hicho Prof. Ibrahimu Lipumba, amewataka wananchi wilayani Kyerwa mkoani Kagera kumchagua kuwa Rais wa Tanzania ili kuweza kuboresha uchumi wao kupitia kilimo,biashara na uvuvi.
Lipumba ameyasema hayo kwenye mkutano wake wa kampeini za kuomba kuchaguliwa leo septemba 24,mwaka huu katika mji mdogo wa Nkwenda wilayani humo ambapo amesema wilaya ya Kyerwa ni wilaya ambayo imebahatika kuwa na ardhi yenye rutuba ambayo inaweza kustawisha mazao ya aina yote japo wananchi wa wilaya hiyo bado wanalia na umasikini.
Amesema kuwa ubora wa ardhi na uwepo wa mipaka ya Tanzania na Uganda pamoja na Rwanda inatakiwa kuwa fursa kwa watanzania waishio maeneo hayo katika kuchochoe maendeleo yao kwa kutafutiwa masoko ya mazao wanayoyalima badala ya kuyauza mazao hayo kwa njia ya magendo.
“Ndugu zangu wa Kyerwa niwaombe mnichague mimi na chama changu ili niweze kutengeneza serikali yenye kuinua uchumi wa kila mtanzania kama ilivyo ahadi ya chama chetu ya kuwa haki sawa kwa wote, wilaya hii wananchi wake hamtakiwi kuwa masikini wala kulia kwa changamoto ya kukosa maji safi na salama pamoja na miundombinu ya bara bara wakati mnazo rasilimali nyingi za kuwainua.” Amesema Prof. Lipumba.
Ameongeza kuwa wilaya ya Kyerwa inalima sana Kahawa na ndizi lakini masoko yake hayawalipi wakulima na kuongeza kuwa endepo atapewa ridhaa ya kuongoza Tanzania atahakikisha kwanza anazijenga barabara zote za wilaya hiyo kwa kiwango cha lami ili kuweza kuunganisha nchi jilani na kuifanya Kyerwa kuwa kitovu cha biasha hasa ya mipakani.
“Octoba 28, mwaka huu ni siku muhimu ya kuamua mustakabali mzima wa maisha yenu, naombeni kura na nitakapokuwa Rais nitaanza na barabara hii ya kwenda mpakani kwa kiwango cha kimataifa ili iwe kichocheo cha uchumi wa watu wa Kagera lakini na kuweza kuongeza uchumi wa nchi kwa ujumla na uzuri mimi ni mwananuchumi wa kimataifa.” Amesema Lipumba.
Prof. Lipumba ameanza ziara yake ya kuomba kura kwa kufanya mikutano mkoani Kagera ambapo jana alikuwa wilayani Muleba na leo anafanya mikutano ya kampeini katika wilaya za Kyerwa na Karagwe.