Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga mkoa wa Dodoma,Bruno Mponzi ,akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma wakati akipinga upotoshaji uliotolewa na mgombea mwenza wa CHADEMA Salum Mwalimu kuhusu vitambulisho vilivyotolewa na Rais Dkt.Magufuli kwa wamachinga.
Baadhi ya wamachinga wakimsiliza Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga mkoa wa Dodoma,Bruno Mponzi, wakati akitoa tamko juu ya upotoshaji uliotolewa na mgombea mwenza wa CHADEMA Salum Mwalimu kuhusu vitambulisho vilivyotolewa na Rais Dkt.Magufuli kwa wamachinga.
Mwenyekiti wa Wamachinga Soko la jioni Nyerere Square Baraka Mrisho,akisisitiza jambo wakati akitoa ufafanuzi wa kauli iliyotolewa na Mgombea mwenza wa CHADEMA juu ya Vitambulisho vilivyotolewa kwa machinga na Rais Dkt.Magufuli.
Mfanyabiashara katika Stendi Kuu jijini hapo, Makubi Salehe,akitoa pongezi kwa Rais Dkt.Magufuli kwa kuwajali na kuwathamini kwa kuwapa vitambulisho vinavyowafanya wawe huru na kuwambia Mgombea mwenza wa CHADEMA apambane na hali yake na sio kuwaingiza wamachinga katika siasa wao chaguo lao ni Dkt.Magufuli
Mamalishe Dodoma Dodoma Square Elina Michael,akielezea jinsi alivyonufaika na Vitambulisho walivyopewa na Rais Dkt.Magufuli
………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Wafanyabiashara wadogo wadogo Mkoani Dodoma (Wamachinga) wamekanusha na kutoa onyo kali kwa taarifa iliyotolewa na mgombea mwenza wa CHADEMA Salum Mwalimu kuhusu vitambulisho walivyopewa na Rais John Magufuli kuwa wamedhurumiwa na kuibiwa.
Wakitoa tamko hilo leo jijini Dodoma wamesema kuwa wanapinga upotoshaji huo uliotolewa jana na Salum Mwalimu kuhusu vitambulisho katika mkutano wa hadhara Isaka, Kahama mkoani Shinyanga.
Akiwa katika Mkutano huo Salumu Mwalimu alisema kuwa vitambulisho vya ujasiriamli ni wizi mtupu wamachinga wameibiwa na wamedhurumiwa kwa kununua vitambulisho hivyo Sh 20,000.
Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga mkoa wa Dodoma,Bruno Mponzi amesema watu wanapaswa kuzipuuza taarifa hizo kwani hazina ukweli wowote na kuwa wana imani kubwa na kiongozi wao Rais Dkt.Magufuli kwa kuwajali na kuwathamini.
“Wasitafutie kura kwa wamachinga, kwani Rais Magufuli amewathamini kiasi cha kutosha na wanaahidi kwamba ifikapo Oktoba 28, watampigia kura na kauli yao ni ‘Wamachinga na Magu miaka mitano tena,” amesema Mponzi
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wamachinga Soko la jioni Nyerere Square Baraka Mrisho amesema kuwa wanaipongeza serikali kwa kuwathamini wamachinga kwa kutoa vitambulisho hivyo kwani vimekuwa ni msaada mkubwa katika biashara zao.
”Vitambulisho hivi vimekuwa mkombozi kwetu na vimetupa heshima kubwa mno hivyo tunataka wanasiasa wasitutumie sisi wamachinga kutafuta kura na kama mtaji wa kisiasa kwao”amesema Mlisho
Aidha Mlisho amesema kuwa wanasiasa hao wanatakiwa kuacha kuwatumia wamachinga kama mtaji wa kutafuta kura, waache kwani wao wanaona vitambulisho hivyo kwao vimewapa heshima kubwa na vimeondoa ushuru waliokuwa wakitozwa.
Naye Mfanyabiashara katika Stendi Kuu Nanenane,Makubi Salehe amesema kuwa hawajahujumiwa kwa kupewa vitambulisho kwa sh 20,000 kwani hapo awali walikuwa wakilipa fedha nyingi na hawakuheshimika lakini sasa wanafanya biashara kwa uhuru.
Nao Mamalishe Nyerere Square jijini hapo Chiku Shomari pamoja na Elina Michael wamesema kuwa vitambulisho hivyo vimewaheshimisha wanaheshimiwa wamekuwa kama maofisa wanaotoka ofisini hata kama wao ni mamalishe.
Hivyo wamewataka wanasiasa watafute kura sehemu nyingine na sio kwao bila kuwatumia wamachinga ambao wanajua wazi Rais Magufuli amewaheshimu kwa kuwapa vitambulisho hivyo na sasa wanafanya biashara kwa uhuru mahali popote.