***************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya imepokea vifaa tiba vya kujikinga na Corona pamoja na taulo za kike (Sanitary Pads) kwaajili ya waathirika wa dawa za kulavya.
Umoja wa Nchi za Ulaya kupitia mradi wa EU-ACT wametoa mashine 12 za kunawia mikono pamoja na sabuni zake kwa vituo vya Methadone nchini. Pia Mwanamitindo Mtanzania Flaviana Matata kupitia taasisi ya Faviana Foundation wametoa taulo za kike kwa wanawake wanaopata nafuu kutokana na matumizi ya dawa za kulevya waliopo kwenye nyumba za upataji nafuu (Sober house) kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Ameyasema hayo leo Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya, James Kaji kwenye utoaji wa misaada hiyo uliofanyika kwenye ofisi za Mamlaka hiyo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Wanahabari Jijini Dar es Salaam, Kamishna Jeneral James Kaji amesema mpaka sasa kuna jumla ya nyumba 29 za upataji nafuu (Sober houses), kati ya hizo ni nyumba tatu zinahudumia wanawake,
“Nyumba za upataji nafuu ambazo zinahudumia wanawake zipo katika Mikoa ya Kilinjaro (Hai), Pwani (Bagamoyo) na Dar es Salaam (Kigamboni) na zinajumla ya wanawake 35”. Amesema Kamishna Jenerali Kaji.
Kwa upande wake Mwanamitindo Bi.Flaviana Matata amesema wameamua kutoa taulo za kike bure ambazo zitawasaidia wanawake waliopo kwenye nyumba za upataji nafuu (Sober houses) katika kipindi cha mwaka mmoja.
“Tulifuatwa tukaambiwa kuna changamoto ya taulo za kike kwenye sober houses hapa Dar es Salaam pamoja na Arusha, tukapewa idadi ya wanawake wenye uhitaji na tukaamua kuanza kuwasaidia wanawake kupata taulo zetu za kike bure kwa mwaka mzima”. Amesema Flaviana Matata.