Msajili wa Hazina Athumani Selemani Mbutuka akizungumza wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya watendaji wakuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) yaliyofanyika katika Ukumbi wa TBA, jijini Dodoma, wa Kwanza aliyeketi kulia ni Postamasta Mkuu wa TPC, Hassan Mwang’ombe akifuatiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TPC Kanali Mstaafu Dkt. Haruni Kondo.
Msajili wa Hazina Athumani Selemani Mbutuka (walioketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wakuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) kushoto walioketi ni Postamasta Mkuu wa TPC, Hassan Mwang’ombe akifuatiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TPC Kanali Mstaafu Dkt. Haruni Kondo na Kulia walioketi ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mawasiliano Caroline Kanuti wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasilano) akifuatiwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara hiyo, Kitolina Kippa.
Msajili wa Hazina Athumani Selemani Mbutuka akimpa mkono wa pongezi Meneja wa TPC Mkoa wa Mtwara aliyebuni wazo la Posta kuwa wakala wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya watendaji wakuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) yaliyofanyika katika Ukumbi wa TBA, jijini Dodoma, wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya TPC Kanali Mstaafu Dkt. Haruni Kondo.
Meneja Mkaazi , Zanzibar wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Khamis Ahmed Swedy, akimpa mkono wa shukurani Msajili wa Hazina Athumani Selemani Mbutuka kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi na kufunga mafunzo ya siku tano ya watendaji wakuu wa Shirika hilo yaliyofanyika katika Ukumbi wa TBA, jijini Dodoma wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasilano) Kitolina Kippa akifuatiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mawasiliano katika Wizara hiyo Caroline Kanuti.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasilano) Kitolina Kippa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Sekta hiyo kabla ya kufungwa rasmi mafunzo ya siku tano ya watendaji wakuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) yaliyofanyika katika Ukumbi wa TBA, jijini Dodoma, waliokaa kuanzia kushoto ni Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe akifuatiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TPC Kanali Mstaafu Dkt. Haruni Kondo akifuatiwa na Msajili wa Hazina Athumani Mbutuka.
*******************************
Na Faraja Mpina, WUUM, Dodoma
Msajili wa Hazina Athumani Selemani Mbutuka ameliagiza Shirika la Posta Tanzania (TPC) kubadilika katika utendaji wao kulingana na ushindani uliopo na mashirika mengine, kwa kuwa wabunifu kibiashara na kuweka malengo ya kuongeza ukusanyaji wa mapato hasa katika biashara yake ya duka la kubadilisha fedha (Bureau de change) ili kuhakikisha wanaongeza uzalishaji, na uchumi wa Shirika hilo unaimarika ili kuweze kutoa gawio kubwa kwa Serikali.
Mbutuka aliyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tano ya viongozi wakuu wa Shirika hilo yaliyofanyika katika ukumbi wa TBA jijini Dodoma.
“Ili uingine katika ushindani ni lazima uwe na uwezo wa kushindana kwa kuzingatia fursa zilizopo, mahitaji ya wateja na ukuaji wa teknolojia, hasa kipindi hiki cha matumizi ya TEHAMA katika kutoa huduma mbalimbali kwa jamii. Shirika hili limepewa dhamana ya kutoa huduma nyeti na muhimu kwa Serikali na jamii, hivyo linatakiwa kuwa Shirika la mfano na lijiendeshe kwa faida kwa kuhakikisha kila tawi la Posta nchini linatoa huduma bora na kuzalisha faida kwa Shirika na kuweza kutoa gawio kubwa zaidi kwa Serikali”, alizungumza Mbutuka.
Aliongeza kuwa mafunzo waliopata viongozi wakuu wa Shirika hilo ni mtaji mzuri kwa viongozi na yapelekwe kwa wafanyakazi walio chini yao ili kuboresha utendaji, kuongeza uzalishaji, ufanisi na ubunifu katika kutoa huduma kwa jamii na kutimiza malengo ambayo Shirika limejiwekea ya kujiimarisha kiutendaji na kiuchumi.
Mwenyekiti wa Bodi ya TPC Kanali Mstaafu Dkt. Haruni Kondo ametoa rai kwa watendaji wa Shirika hilo kushikana pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili kulinda nafasi zao na kuikusanyia Serikali mapato stahiki kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Shirika hilo la kuhudumia wananchi na Serikali.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Kitolina Kippa akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amewataka Meneja wa Mikoa na Kanda wa Shirika hilo kuboresha mahusiano mahala pa kazi kwa kuheshimu mamlaka zilizo juu yao ili na watendaji walio chini yao wawaheshimu na kuepusha migogoro ambayo inapunguza utendaji wa kazi na uzalishaji.
“Mafunzo haya yawe chachu ya mabadiliko katika utendaji wenu huku mkitambua kuwa cheo cha Umeneja sio kuwa Bosi, ni utendaji, hivyo mkafanye kazi kwa bidii na kuzalisha faida kupita malengo yaliyowekwa na Shirika”, Alizungumza Kippa.
Postamasta Mkuu wa TPC Hassan Mwang’ombe amesema kuwa Shirika hilo sasa lipo katika harakati za kuanza kutoa huduma kidigitali na tayari limekwishandaa mfumo maalumu wa kutolea huduma unaoitwa Postal Management Information System (PMIS) na huduma za Posta zitaingizwa ndani ya mfumo huo, ambapo mpaka sasa mfumo wa malipo wa MUSE, EMS na barua tayari vimeshaingizwa katika mfumo huo.
Katika hatua nyingine Mwang’ombe amempongeza Meneja wa TPC Mkoa wa Mtwara kwa ubunifu wa kuleta wazo la Shirika hilo kuwa Wakala wa huduma za kibenki na Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ), ambapo tayari uzinduzi wa ushirika huo umekwishafanyika na kwa kuanzia huduma za PBZ zitaanza kutolewa na TPC katika mikoa nane Tanzania bara na baadae nchi nzima. Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaasa Meneja wake kuwa wabunifu katika kutoa huduma za Posta nchini.