Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa daraja la mto Mara linalounganisha Wilaya ya Serengeti na Tarime, mkoani Mara, Septemba 20, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa Kata ya Matongo, Wilaya ya Tarime vijijini katika mkutano wa kampeni uliyofanyika kwenye viwanja vya Nyamongo Sekondari, Septemba 20, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
*************************************
“Hiki siyo kipindi cha kujutia maamuzi au cha kufanya majaribio ya uongozi. Chagua kiongozi mwenye uwezo wa kungoza nchi. Usimchague mtu tu hata kama ni mtoto wa dada yako.”
Kauli hiyo imetolewa jana jioni (Jumamosi, Septemba 19, 2020) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata za Issenye na Natta waliojitokeza njiani kumlaki wakati akielekea Mugumu, Serengeti, mkoani Mara kuwanadi wagombea wa CCM.
“Tunataka kiongozi atakayelinda rasilmali za Taifa hili. Na huyo si mwingine bali ni Dkt. John Pombe Magufuli. Tunataka kiongozi atakayeweza kuongoza nchi. Wewe mwanachama wa chama rafiki iwe ACT, CHADEMA, NCCR au CHAUMA, mchague Dkt. John Pombe Magufuli awe Rais kwa sababu maendeleo hayachagui chama,” alisema.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia mikutano hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Serengeti, Bw. Amsabi Jeremiah Mhimi na wagombea udiwani wa kata za Issenye na Natta, Bw. Mosi James Nyarobi na Bw. Juma Porini.
Akielezea ni kwa nini anawaomba kura wananchi wa vyama vyote bila kujali itikadi zao za kisiasa, Mheshimiwa Majaliwa alisema: “Ni kwa sabau tunatafuta kiongozi wa nchi. Uongozi wa nchi unataka mtu mwenye busara mweledi, mchapakazi na mwenye nia ya kuleta maendeleo kwa Watanzania, na huyu si mwingine bali ni Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.”
Alisema moja ya sifa za Rais wa nchi ni lazima awe na uwezo wa kulinda tunu za Taifa na moja ya tunu hizo hizo ni amani. “Mgombea urais anayeweza kati ya wote hawa niliowaona, ni Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Tarehe 28 Oktoba ikifika, nenda kampigie kura,” aliongeza.
Akielezea mambo yaliyofanyika kwenye sekta ya afya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilihakikisha Watanzania hawalipi gharama nyingi kwa ajili ya matibabu na ndio maana iliboresha huduma hiyo kuanzia ngazi ya zahanati ili wananchi wapate huduma za afya kwa karibu zaidi.
Katika wilaya ya Serengeti, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 1.7 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo ambapo majengo ya huduma ya mama na mtoto, utawala, kusubiria wagonjwa, OPD na njia ya waendao kwa miguu yalijengwa. Alisema majengo yote hayo yamekamilika na yanatumika.
“Vilevile, shilingi milioni 429 zimetolewa kwa ujenzi wa kituo cha afya Natta, ujenzi wa wodi ya wazazi, wodi ya watoto, maabara, jengo la X-Ray, nyumba ya kuhifadhia maiti na nyumba ya watumishi (6 in 1). Ujenzi umekamilika na majengo hayo yanatumika,” alisema.
“Kuhusu ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, wilaya hii ilipokea shilingi bilioni 1.5. Kila mwezi, zimekuwa zikiletwa fedha za dawa za wastani wa shilingi milioni 30.9,” amesema.
Alisema Halmashauri ilipewa gari moja la kubebea wagonjwa ambalo lilipelekwa kwenye kituo cha afya cha Natta na linafanya kazi.