*************************************
Na.Samwel Mtuwa – Geita.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) Dr Mussa Budeba pamoja na Kamishna Msaidizi wa Mpango wa Ushirikishwaji wa Wazawa katika sekta ya Madini nchini Terence Ngole wafanya mazungumzo maalum jinsi ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wa Madini nchini.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita Dr. Budeba alielezea juu ya umuhimu wa kuweka kipaumbele katika Mpango wa Ushirikishwaji wa Wazawa katika sekta ya Madini ili kulinda uchumi wa nchi kwa kutoruhusu makampuni kutoka nje ya nchi kufanya shughuli zote za uchumi zinazoweza kufanywa na Wazawa.
Akizungumzia kuhusu maonesho ya Madini yanayoendelea mkoani Geita Dr.Budeba alishauri mikoa mingine iige mfano wa Geita kwani Mpango huu wa maonesho ya Madini unaleta tija katika uchumi wa taifa.
Akielezea juu ya Mpango huo Kamishna Msaidizi wa Mpango wa Ushirikishwaji Terence Ngole alisema kuwa ameandaa mkutano na taasisi za fedha na Migodi juu ya kutangaza mahitaji yao na kujua gharama zake kutoka kwa mdhabuni wa nje na ndani ili kupata idadi ya dhabuni zinazoweza kutolewa na makampuni ya wazawa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel alisema kuwa anampango wa kufungua kanzidata juu ya ushirikishwaji wa Wazawa katika sekta ya Madini akishirikisha Taasisi za fedha kwa lengo la kuwasaidia wazawa kwa kuwaboreshea mitaji yao wakiwemo wafanya biashara na wachimbaji wadogo wa Madini.
Akizungumzia juu ya wachimbaji wadogo kufanyiwa Utafiti , Mkuu wa Mkoa alisema yupo tayari kutoa eneo la Uwanja kwa GST ili kuweza kujenga Maabara ya Uchenjuaji Madini kwa lengo la kuwasaidia wachimbaji wadogo kufanya uchimbaji wa kisasa.
Kikao hiki cha ndani kilijumuhisha pia watendaji wengine kutoka GST na Tume ya Madini.