…………………………………………………………………..
Katika siku za hivi karibuni kumeibuka baadhi ya waajiri wasiozingatia Sheria za Kazi kwa makusudi kwa kisingizio kwamba hawawajibiki chini ya Sheria hizo. Waajiri hao wamekuwa hawatoi ushirikiano kwa Maafisa Kazi wanapotekeleza majukumu ya kusimamia utekelezaji wa Sheria za Kazi katika maeneo ya kazi. Aidha, waajiri hao wamekuwa wakitoa taarifa potofu kwa Umma, Viongozi wa Serikali na Wanajumuiya wao kwa lengo la kudhoofisha juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha kuwa Sheria za Kazi zinafuatwa na kuzingatiwa nchini. Ninapenda kuwakumbusha na kuwasisitiza waajiri wote kwamba wanapaswa kuzingatia na kutekeleza matakwa ya Sheria za Kazi.
Ninatoa rai kwa waajiri wote nchini kutoa ushirikiano kwa Maafisa Kazi wanapotekeleza majukumu yao ya kusimamia utekelezaji wa Sheria za Kazi. Aidha, iwapo kuna changamoto yoyote katika utekelezaji wa Sheria, ninawasihi kuwasiliana na Ofisi yangu badala ya kutoa taarifa potofu kwa Umma, Viongozi wa Serikali na Wanajumuiya wao.
Ninaomba kuwahakikishia waajiri wote kuwa, Serikali yetu inathamini Sekta zote ikiwemo Sekta Binafsi na Sekta ya Umma pamoja na Uwekezaji unaofanywa nchini kwa ustawi wa Taifa letu.
IMETOLEWA NA
JENISTA J. MHAGAMA (MB)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU
19 SEPTEMBA, 2020