Na Mwandishi wetu Mihambwe
Shule ya Msingi ya Kitama iliyopo Kijiji cha Kitama Shuleni kata ya Kitama Tarafa ya Mihambwe yawa shule ya mfano kwa ujenzi wa vyoo bora na vya kisasa.
Shule hiyo ilipewa fedha Tsh. 37,778,000/= ya mradi wa SWASH ambapo imejenga vyoo tundu 15 kwa ajili ya Wasishana, tundu 12 kwa ajili ya Wavulana na tundu 2 kwa ajili ya Waalimu vikiwa na mifumo ya maji yanayotoka. Pia ina sehemu maalum kwa ajili ya vyoo vya Walemavu na na vya kumsitiri Mtoto wa kike na kuondoa kabisa uhaba wa vyoo uliokuwepo.
Akiwa kwenye ziara ya kukagua ujenzi miradi ya kimaendeleo, Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli kwa kuwapa fedha hizo ambazo zimeenda kuboresha miundombinu ya vyoo na kutatua changamoto iliyokuwepo.
“Tarafa ya Mihambwe tunasimamia ipasavyo fedha zote za miradi kwa kuhakikisha inaendana na thamani ya fedha. Kwa mara nyingine tunamshukuru Rais Magufuli kutupatia fedha hizi na niwapongeze wote kwa kazi nzuri na ya mfano Kitaifa. Jukumu letu Serikali ni kutekeleza ilani ya uchaguzi CCM kwa kuwaondolea kero na shida Wananchi.” Alisema Gavana Shilatu.
Wananchi wa maeneo jirani wameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa inayowaondolea kero na changamoto zao.
“Naipongeza Serikali ya CCM kwa kuwa wasikivu wa kututatulia shida zetu kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ipasavyo, Mwenyezi Mungu ambariki sana Rais Magufuli” alisema Said Mng’oko mkazi wa kata ya Kitama.
Gavana Shilatu anaendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya kimaendeleo kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa gharama inayolingana na thamani ya fedha husika