Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akizungumza wakati alipofungua kongamano la pili la Kitaifa la Kuzuia Upotevu wa Mazao Baada ya Mavuno mjini Morogoro leo
Bw.Felix Bachmann Mkurugenzi Mkazi wa shirika la HELVETAS nchini akizungumza wakati wa kongamano la pili la Kuzuia Upotevu wa mazao ambapo amesisitiza matumizi ya teknolijia zitakazopunguza matumizi ya kemikali kwenye uhifadhi wa mazao .
Sehemu ya washiriki wa kongamano la pili la Kitaifa la Kuzuia Upotevu wa Mazao Baada ya Mavuno linalofanyika chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Morogoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wadau wa Kilimo Wasio wa Kiserikali (ANSAF) Audax Rukonge akizungumza kwenye kongamano la kitaifa la kuzuia upotevu wa mazao ambapo ameiomba seriklai kuweka mazingira wezshi kwa viwanda vingi kuanzishwa ili kuchakata mazao yatakayosaidia kupunguza hasara ya upotevu kwa wakulima.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Prof.Raphael Chibunda amsema upotevu wa mazao katika nchi za kiafrika ni mwendelezo wa matatizo ambayo waliotutawala walituachia na sasa hatujapata suluhisho hivyo ametoa wito kwa watafiti kujikita kutafuta suluhisho hususan kwenye vyuo vikuu nchini.
*******************************
Serikali imesema wananchi waendelee kufanya kazi zao bila hofu kwa kuwa nchi ina chakula cha kutosha licha ya kuwa na uwezekano wa kutokea mvua kidogo msimu ujao.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya leo (18.09.2020) wakati alipofungua kongamano la pili la Kitaifa la Kuzuia Upotevu wa Mazao baada ya Mavuno linalofanyika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Morogoro.
Tunacho chakula cha kutosha hata endapo mvua ikipungua kwa misimu ujao , serikali imejipanga kukabiliana na upungufu huo hivyo wananchi endeleleni kufanya kazi kwa bidii na kutunza chakula mlichonacho.
“Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imejipanga vizuri katika kuhakikisha kuwa maeneo hayo, yanakuwa na chakula kwenye masoko yao. Nitoe rai kwa watanzania kutumia vizuri chakula kilichopo ili kuondoa upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza” alisema Kusaya.
Katibu Mkuu huyo alisema uzalishaji wa chakula nchini Tanzania, unatosheleza mahitaji ya taifa na kuwa hali ya chakula mwaka huu ni nzuri, kutokana na uzalishaji mzuri katika msimu wa 2019/2020.
Kusaya aliendelea kusema tathmini iliyofanyika hivi karibuni ya msimu wa 2019/2020, inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula unatarajia kufikia tani 17,742,388 ambapo mahitaji ni tani 14, 347,955.
“Nchi inategemewa kuwa na ziada ya tani 3, 511,620 za chakula ambapo tani 1, 322,020 ni za mazao ya nafaka na tani 2, 072,413 ni za mazao yasiyo nafaka” alisitiza Kusaya.
Jitihada nyingine za serikali katika kuhakikisha nchi inakuwa na chakula za kutosha ni kuendelea kununua mazao ya nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ambapo tayari tani 100,000 za mazao zimekwisha nunuliwa ikiwemo mahindi na mpunga.
Kuhusu suala la upotevu wa mazao Wizara ya Kilimo imewashukuru wadau wa sekta ya kilimo kwa kuandaa kongamano hilo ili kujadili mikakati ya kudhibiti wa upotevu wa mazao baada ya mavuno ambao unaathiri uchumi wa wakulima, alisema Kusaya.
Akizungumzia hali ya upotevu wa mazao baada ya mavuno nchini,Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Kitaifa la Kusimamia Udhibiti wa Mazao wanaosimamia mazao baada ya Mavuno (TPMP) Julius Wambura alisema takwimu zinaonesha asilimia 30 hadi 35 ya mazao ya nafaka hupotea wakati wa mavuno na baada ya kuvunwa shambani.
“ Jumla ya gunia 3 hadi 3.5 kati ya 10 zinapovunwa zinapotea shambani au baada ya kufikishwa ghalani hali inayowatia umasikini wa kipato wakulima wetu na kuwapunguzia tija” alisema Wambura.
Aidha alitoa wito kwa wadau wa kilimo kutafuta mbinu na teknolojia rahisi kuwasaidia wakulima kutoendelea kupoteza mazao yao ili kuwa na uhakika wa chakula na kipato.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Prof.Raphael Chibunda alisema upotevu wa mazao katika nchi za kiafrika ni mwendelezo wa matatizo ambayo waliotutawala walituachia na sasa hatujapata suluhisho .
Alikemea tabia wa watafiti wakiwemo kwenye vyuo vikuu kutofanya tafiti za kusaidia wakulima kuondokana na tatizo la upotevu wa mazao kwani vyuo vingi havifundishi wanafunzi kukabiliana na tatizo hilo
“ Tunafanya tafiti nyingi lakini haziendi kutatua kero za upotevu wa mazao shambani.Nchi hii inakula ugali lakini hakuna maprofesa wa ugali,wengi waliopo wamebobea kwenye biskuti “alisema Prof.Chibunda.
Prof.Chibunda alitoa wito kwa mamlaka za udhibiti kama TMDA,TBS,Polisi kusaidia wakulima nchini kuwa na uhakika wa kusafirisha mazao yao na kupunguza vikwazo kwa wakulima ili mazao yasiharibike kabla hayajafika sokoni au ghalani.
Akizungumza kwa niaba ya wadau wa kilimo,Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Wadau wa Kilimo Wasio wa Kiserikali (ANSAF) Audax Rukonge alisema anaiomba serikali iendelee kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa teknolojia rahisi ya kuchakata na kuhifadhi mazao ili wakulima wapate faida hali itakayosaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Kongamano hili linafanyika mara ya pili kwa lengo la kujadili mikakati ya kusaidia kudhibiti upotevu wa mazao baada ya mavuno ambapo lilikuwa lifanyike mwezi Februari mwaka huu lakini likaahirishwa kutokana na janga la korona.
Aidha kongamano hili ni matokea ya uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mazao Baada ya Kuvuna (2019-2029)ulizinduliwa Agosti 2019 na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maonyesho ya Sikukuu ya Wakulima Nane nane, iliyofanyika mkoani Simiyu.