**************************
NJOMBE
Serikali mkoani Njombe imejinasibu kwamba imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kutoka vifo 32 hadi kufikia vifo 10 kwa mwaka na kuahidi kuendelea kuoberesha miundombinu ili kukomesha kabisa tatizo hilo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya hospitali ya mji w Njombe Kibena iliyokuwa chini ya mkoa ikitumika kutoa huduma za rufaa kwa kipindi cha mwaka mmoja mkuu wa mkoa w Njombe mhandisi Marwa Rubirya amesema tangu 2015 katika hospitali ya Kibena kulitokea mikasa ya vifo zaidi ya 30 vya akina mama na kwamba kitendo cha kupandisha hadhi hospitali hiyo mwaka mmoja uliopita kuwa rufaa imesaidia kuboresha huduma na kunusuru vifo vingi.
Rubirya amesema kipindi chote ambacho hospitali hiyo ilitumika kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa serikali imeongeza madaktari wabobezi wakutosha,Vifaa tiba, Dawa na Majengo muhimu kama jengo la Upasuaji na X rays na kuweka bayana mpango wa kutokomeza kabisa vifo vya akina mama na watoto.
Awali mganga mfawidhi hospitali ya rufaa mkoa wa Njombe Dr Wilfred kyambile anasema wakati mkoa unakabidhiwa hospitali hiyo ilikuwa katika hali mbaya lakini wameweza kupunguza vifo kutokana na maboresho ya huduma na kisha kuongeza mapato.
Akipokea nyaraka wakati wa makabidhiano mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe Illuminata Mwenda anasema kurejeshwa kwao hospitali hiyo kutawafanya kuongeza makusanyo na kuahidi kuitunza na kuendelea kuboresha matibabu.
Hospitali ya mji Kibena iliyokuwa ikitumika kutoa huduma za rufaa ikiwa chini ya mkoa imerejeshwa halmashauri ya mji wa Njombe baada ya serikali kukamilisha ujenzi wa hospitali ya rufaa.