Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo anasikitika kutangaza kifo cha Afisa Mkuu Brigedia Jenerali Nelson Hosea Msanja (mstaafu)
Brigedia Jenerali Msanja (Mstaafu) aliaga dunia tarehe 10 Septemba, 2020 katika Hospitali ya Life Groenkloof nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu.
Marehemu alizaliwa tarehe 01 Julai, 1958 katika Kijiji cha Utemini, Tarafa ya Utemini, Wilaya ya Singida Mkoa wa Singida. Alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tarehe 19 Disemba 1979.
Katika utumishi wake Jeshini marehemu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Kaimu Mkuu wa Tawi la Ukaguzi Jeshini (2013 – 2015); Kamishna wa Utafiti na Maendeleo ya Jeshi Wizara ya Ulinzi na JKT (2015-2017); Kaimu Mkuu wa Tawi la Uhandisi na Logistiki Jeshini (2017) na Mwambata Jeshi nchini Afrika Kusini hadi alipostaafu kwa heshima tarehe 30 Juni 2020.
Brigedia Jenerali Msanja (Mstaafu) alitunukiwa medali zifuatazo katika miaka 40 na miezi sita ya utumishi wake: Vita ya Kagera; Miaka 20 ya JWTZ; Utumishi mrefu; Miaka 40 ya JWTZ; Utumishi Uliotukuka; Nishani ya Comoro; Miaka 50 ya Uhuru; Miaka 50 ya Muungano na Miaka 50 ya JWTZ.
Mwili wa Marehemu utawasili nchini kwa ndege ya JWTZ tarehe 17 Septemba, 2020 na kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo (521KJ).
-2-
Heshima za mwisho kwa marehemu zitatolewa katika eneo la kuagia la Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo tarehe 18 Septemba, 2020. Kuanzia saa 3:00 asubuhi na mazishi yatafanyika tarehe 19 Septemba, 2020 nyumbani kwake Chanika Mwisho Jijini Dar es Salaam.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi Amina.