………………………………………………………………………..
Na Shamimu Nyaki – WHUSM
Sekta ya Filamu nchini imeendelea kuwa mhimili katika ukuaji na maendeleo ya uchumi wa watanzania na Taifa kwa ujumla. Sekta hii imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha na kuendeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda ambao umeifanya Tanzania nchi ya Uchumi wa Kati.
Serikali kupitia Bodi ya Filamu imeendelea kuhakikisha wanatasnia wa Filamu wanashiriki vyema katika kufikia azma hiyo kwa kutengeneza ajira, mapato na kuchangia maendeleo ya sekta nyingine kama vile utalii, uchukuzi na usafirishaji.
Bodi ya Filamu imeendelea kuhakikisha kuwa maudhui ya filamu zinazopelekwa katika masoko ya ndani zilizotayarishwa na watengenezaji kutoka ndani na nje ya nchi zinahakikiwa na kuzipangia madaraja kwa ajili ya kuzingatia taratibu za kisheria kabla hazijapelekwa sokoni au kwa walaji kupitia mifumo na njia mbalimbali.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Dkt. Kiago Kilonzo kupitia semina na warsha mbalimbali alizotoa kwa wadau wa sekta hiyo anasema yapo mambo mbalimbali ambayo yameleta mafanikio makubwa katika tasnia hii ambayo yameleta tija kwa wadau na taifa kwa ujumla.
Mafanikio hayo ni pamoja na ongezeko la vibali vya utayarishaji wa filamu ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Mei, 2019, Vibali 620 vilikuwa vimetolewa. Kati ya vibali hivyo, vibali 480 vilitolewa kwa watengenezaji kutoka nje ya nchi na vibali 140 kwa watengenezaji watanzania.
“Katika Awamu ya Tano jumla ya picha jongevu (filamu) zilizohakikiwa zimeongezeka kutoka filamu 1331 kwa mwaka 2015/2016 hadi filamu 3,620 kwa mwaka 2019/2020 hadi mwezi Mei, 2020. Kati ya filamu hizo, filamu 3079 zilikuwa za watayarishaji wa ndani kitanzania na filamu 541 kutoka nje ya nchi” alisema Dkt.Kilonzo.
Hata hivyo, Bodi ya Filamu imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha utendaji katika sekta hii ikiwa ni pamoja na kurasimisha shughuli na biashara za filamu ikiwemo miundombinu ya usambazaji, utayarishaji na uoneshaji wa Filamu. Aidha, utaratibu wa kuwatambua waigizaji, waandishi wa miswada, watayarishaji, wachekeshaji, waongozaji na wasambazaji unaendelea kwa kuwapatia vitambulisho vinavyotolewa kwa kuzingatia kada zao.
Mathalani kupitia wadau mbalimbali wakiwemo DSTV, AZAM Media, Kampuni ya Steps Entertainment, Pilipili Entertainment wamekuwa mstari wa mbele kutoa ajira kwa wasanii wengi kupitia miradi ya utayarishaji wa tamthilia mbalimbali. Baadhi ya tamthilia hizo ni pamoja na Kapuni, Huba, Slay Queen, Nyavu, Sarafu, Tandi, Single Mama, Shiingi, Panguso na Uhuru una gharama zake.
Katika kutekeleza majukumu yake, Bodi imeendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wadau wake ikiwemo Vyama na Mashirikisho mbalimbali ya watendaji na wadau wa Sekta ya Filamu nchini hatua iliyosaidia kuimarisha Miongozo ya Vyama hivyo na kuwezesha upatikanaji wa Katiba ya Shirikisho la Filamu nchini (TAFF) iliyofanyiwa marekebisho ili kuongeza tija na uwajibikaji kwa maendeleo ya sekta.
Ni wazi maboresho yaliyofanyika yametoa dira imara inayoijenga na kuiimarisha sekta ya Filamu, ni wakati sasa kwa wasanii kuona fursa zilizopo katika tasnia hiyo na kutengeneza kazi bora ambazo zintaendana na soko la Dunia ya leo.
MWISHO.