Home Mchanganyiko Wananchi wakumbushwa kulinda vyanzo vya maji wakati Kata 3 zikinufaika na mradi

Wananchi wakumbushwa kulinda vyanzo vya maji wakati Kata 3 zikinufaika na mradi

0

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akihakikisha upatikanaji wa maji katika vituo vya kutolea maji vilivyojengwa katika kijiji cha Kalumbaleza.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa tatu toka mbele) akiwa na baadhi ya wataalamu wa SUWASA wakati alipotembelea Mradi wa MUZE GROUP katika bonde la Ziwa Rukwa.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo akielekea kwenye chanzo cha maji ya mradi wa MUZE GROUP unaotarajiwa kuhudumia vijiji 10 katika Bonde la Ziwa Rukwa Wilayani Sumbawanga.

*****************************

Wananchi wa Kijiji cha Kalumbaleza na vitongoji vyake katika bonde la ziwa Rukwa, Wilayani Sumbawanga, Mkoani Rukwa wamehimizwa kuendelea kulinda na kutunza vyanzo vya maji vinavyowasaidia kuendelea kupata maji katika kipindi chote cha mwaka ili kuepukana na shida ya kutafuta maji katika umbali mrefu wakati wakisubiri kukamilika kwa mradi wa maji wa MUZE GROUP unaotarajiwa kumalizika mwezi Novemba mwaka huu

Hayo yamesisitizwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipokutana na wananchi baada ya kutembelea mradi huo wa maji utakaohudumia vijiji 10 vya kata 3 za Muze, Mwadui na Kalumbaleza na kuwataka wananchi hao kutolima na kufanya shughuli za kibinaadamu karibu na vyanzo hivyo pamoja na kuilinda miundombinu ya maji inayoendelea kusimikwa katika maeneo mbalimbali ya vijiji hivyo.

Aidha, Mh. Wangabo ametoa tahadhari kwa vijiji vya wilaya ya Nkasi vilivyopo juu ya milima ya Lyamba lyamfipa wanaoendelea kufanya shughuli za kibinaadamu kuacha kufanya hivyo kwani uhai wa Maisha ya watu wa bonde la ziwa rukwa unategemea utunzaji wa mazingira wa wananchi wanaoishi kanda ya juu ya safu za milima hiyo.

“Halafu wale ambao wapo wilaya ya Nkasi vile vijiji viwili, nitawafuata huko huko ili watunze mazingira ninyi huku mpate maji ya uhakika, vinginevyo hii kazi itakuwa kazi bure, kama wale wasipotunza mazingira wanakata miti hovyo kwenye chanzo cha maji ninyi huku hamtapata maji, kuna vijiji viwili vya Nkasi, nitavifuata huko huko juu, lakini ninyi cha hapa chini mtimize wajibu wenu, chini ya mwenyekiti wenu serikali ya Kijiji,” Alisisitiza.

Kwa upande Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Sumbawanga Mhandisi Gibon Nzowa alisema kuwa mradi huo unalenga kuweka vituo 65 pamoja na matenki matano katika vijiji hivyo 10 huku wakitegemea kulaza bomba za kusambazia maji kwa Zaidi ya km 60 na kisha kueleza changamoto zinazokwamisha zoezi hilo.

“Changamoto tuliyokutana nayo mheshimiwa mkuu wa mkoa ni mvua nyingi kipindi cha masika tulikwama kidogo, vile vile changamoto nyingine ni uchafuzi wa chanzo juu katika vijiji vilivyopo wilaya ya Nkasi na kuchelewa kupata fedha kwa wakati,” Alisema.

Mmoja wa wanakitongiji cha katoro katika Kijiji cha Kalumbaleza Emanuel Michael aliiomba serikali kuona uwezekano wa kuwekewa bomba katika kjiji chao ambacho kipo karibu na Kijiji cha Kalumbaleza na kusema “nafikiri wale waliokuja kupima huu mradi, walifika wakapima kule katoro, kule tunakunywa maji ya visima lakini cha ajabu kule hakuna bomba hata moja lakini sisi ni wakazi wa Kijiji cha Kalumbaleza na kata ya kalumbaleza.”

Katika hatua nyingine Mh. Wangabo ameipongeza Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Sumbawanga pamojana Mkurugenzi wake kwa kutoa ajira Zaidi ya 300 katika utekelezaji wa mradi huo huku wakiokoa zaidi ya Bilioni 3 kwa kutarajiwa kuukamilisha mradi huo kwa bilioni 3.1 balaya ya bilioni 6 za awali huku fedha hizo zikitolewa na serikali kwa asilimia 100. Vijiji vitakavyofaidika na mradi huo ni Kalumbaleza A na B, Muze, Mnazi mmoja, Mnazi Asilia, Ilanga, Isangwa, Mbwilo, Uzia na Kalakala.