Aliyepo kushoto ni Mtendaji wa kata ya Kati, Suleiman Kikingo na wa pili yake Ni Mkurugenzi wa Bodi ya maji bonde la Pangani,Segule Segule akizungumza katika kikao kazi hicho kilichowashirikisha watendaji wa mitaa na kata katika jiji la Arusha
Baadhi ya watendaji wa mitaa na kata katika jiji la Arusha wakiwa katika kikao Cha kujadili changamoto za usimamizi wa rasilimali za maji katika jiji la Arusha kilichoandaliwa na Bodi ya maji bonde la Pangani kilichofanywa mjini hapa.(Happy Lazaro)
Baadhi ya watendaji wa mitaa na kata katika jiji la Arusha wakiwa katika kikao kazi Kati ya bonde la Pangani katika kujadili changamoto za usimamizi wa rasilimali za maji katika jiji la Arusha
……………………………………………………………………
Happy Lazaro,Arusha.
Mkurugenzi wa maji bonde la Pangani Segule Segule amesema kuwa, wapo katika mchakato wa kubaini na kuvifuatilia visima vyote ambavyo vimechimbwa pasipo kufuata taratibu na Sheria za uchimbaji.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika kikao kazi Kati ya bonde la Pangani na watendaji wa mitaa na kata katika jiji la Arusha ili kujadili changamoto za usimamizi wa rasilimali za maji katika jiji la Arusha .
Segule alisema kuwa, kumekuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria unaofanywa na wananchi katika shughuli nzima za uchimbaji wa visima ambapo asilimia kubwa ya wananchi wamekuwa wakichimba kiholela bila kufuata sheria zilizopo .
Alisema kuwa ,ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha kuwa wanafuata sheria katika uchimbaji wa visima vya maji ikiwa ni pamoja na kupata vibali vya uchimbaji kutoka mamlaka husika .
Segule amesema visima takribani 300 Bado havijatambulika hivyo wanafanya juhudi za kuzibaini kupitia baadhi ya kata kwa kufanya ufuatiliaji kwa vile visima vilivyochimbwa pasipo kufuata taratibu na sheria katika uchimbaji.
Akimwakilisha Mkuu wa wilaya ya Arusha katika kikao hicho ,Afisa Tawala wa wilaya ya Arusha Nyangusi Nailiba amesema wilaya itafuatilia kwa ukaribu Jambo hilo na kuwachukulia sheria wale wote wanaoenda kinyume na Taratibu za Miongozo ya uchimbaji visima .
Naye Afisa usafi na mazingira jiji la Arusha, James Lobikoki amesema kuwa, semina hiyo imekuja muda muafaka kwani asilimia kubwa ya wananchi wamekuwa hawana uelewa wowote juu ya uchimbaji wa visima ambapo wengi wao wamekuwa wakichimba kiholela tu.
Lobikoki amesema kuwa,kupitia semina hiyo italeta manufaa makubwa na kuwepo kwa usimamizi ulio Bora kwa watendaji wa mitaa na kata ambao watakuwa mabalozi wazuri wa kusimamia kikamilifu uchimbaji huo Huku wakifuata sheria na kanuni zilizopo.
Aliwataka wananchi wa jiji la Arusha kuhakikisha wanatunza kikamilifu mazingira na kuepuka uchimbaji wa visima hovyo ambao umekuwa haufuati sheria na kanuni za uchimbaji.
Baadhi ya watendaji wa kata wakizungumza katika kikao hicho ,Mtendaji wa kata ya Kati halmashauri ya Arusha,Suleiman Kikingo amesema kuwa,kikao hicho kimewafungua wao Kama watendaji ambapo wataenda kuwa mabalozi wazuri katika maeneo yao kwa kutoa elimu juu ya umuhimu wa kufuata sheria na taratibu za uchimbaji wa visima hivyo.