Home Mchanganyiko MAENDELEO YA UJENZI WA HOSPITALI YA UHURU CHAMWINO YAIKUNA AIRTEL TANZANIA

MAENDELEO YA UJENZI WA HOSPITALI YA UHURU CHAMWINO YAIKUNA AIRTEL TANZANIA

0

Mhandisi wa Ujenzi wa jengo la Hospitali ya Uhuru
iliyopo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma, Bw. Girimu Kanansi (kushoto) akieleza
kuhusu ukamilishaji wake ambapo unatarajiwa kumalizika Oktoba mwaka huu. Kulia
ni Afisa Mawasiliano wa Kampuni ya Airtel Tanzania Bw. Jackson Mbando

Muonerkano wa Jengo la Hospitali ya Uhuru iliyopio
Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma, ambao umekamilika kwa asilimia 87 na
unatarajiwa kumalizika Oktoba mwaka huu.
Mhandisi wa Ujenzi wa jengo la Hospitali ya Uhuru
iliyopo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma, Bw. Girimu Kanansi (wa pili kulia) akimuongoza
Afisa Mawasiliano wa Kampuni ya Airtel Tanzania Bw. Jackson Mbando (kulia)
alipotembelea Hospitali hiyo kuangalia maendeleo yake, ikizingatiwa fedha za
mradi huo zilitolewa na Mbia mwenza wa Air tel Tanzania ambaye ni Bharti Airtel
ya India kiasi cha Sh. bilioni 2.3.
Mhandisi wa Ujenzi wa jengo la Hospitali ya Uhuru
iliyopo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma, Bw. Girimu Kanansi (kushoto) na Afisa
Mawasiliano wa Kampuni ya Airtel Tanzania Bw. Jackson Mbando (kulia), wakiwa
katika picha ya pamoja na watumishi wa Kampuni ya Airtel Tanzania, baada ya
kutembelea ujenzi wa Hospitali hiyo.

Afisa Mawasiliano wa Kampuni ya Airtel Tanzania Bw.
Jackson Mbando (kulia), akielekeza jambo alipotembelea moja ya Duka la Kampuni
hiyo lililofunguliwa jirani na linapojengwa jengo la Hospitali ya Uhuru Mkoani
Dodoma, ambapo Kampuni hiyo inamchango wake katika ufanikishaji wa mradi huo.

Ujenzi wa Hospitali ya Uhuru Wilayani Chamwino Mkoani
Dodoma umekamilika kwa asilimia 87 baada ya Serikali kutekeleza ahadi yake ya kuzielekeza
takribani Sh. bilioni 2.3 zilizotolewa na Kampuni ya Bharti Airtel ya India
kujenga Hospitali hiyo.

Hayo yalibainishwa na Mhandisi wa Ujenzi wa jengo la
Hospitali ya Uhuru, Bw. Girimu Kanansi, wakati Afisa Mawasiliano wa Airtel
Tanzania, Bw. Jackson Mmbando, alipotembelea hospitali hiyo kuangalia maendeleo
ya ujenzi wake, Mkoani Dodoma

Bw. Kanansi alisema kuwa jengo hilo lililokamilika kwa
asilimia 87 linajengwa kwa weledi mkubwa na Kampuni ya Suma JKT kupitia vijana
wazalendo wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kinyume na awali ambapo majengo
makubwa kama hayo yalikuwa yanajengwa na kusimamiwa na wageni kutoka nje ya
nchi.

“Kazi inayoendelea ni kutengeneza sakafu, kuweka
mifumo ya umeme na kuskimu kuta, hivyo ninaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano
na Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel kuona umuhimu wa kupeleka huduma za Afya
karibu na wananchi hususani mkoani Dodoma ambako ndio makao Makuu ya nchi”,
alieleza Mhandisi Kanansi.

Alisema kuwa Jengo hilo lilitarajiwa kukamilika mwezi
mei mwaka huu, lakini ilishindikana kutokana na changamoto ya msimu wa mvua
kali ambao ulisababisha kutokuwa na mazingira Rafiki ya kusafirisha vifaa
kwenda eneo la ujenzi.

Aidha kutokana na hali hiyo Mkandarasi aliomba
kuongezewa muda, ambapo anatarajia kukamilisha ujenzi Oktoba mwaka huu iwapo
hakutakuwa na changamoto yeyote itakayojitokeza ikiwemo ya kutofika kwa vifaa
vya ujenzi kwa wakati.

Kwa upande wake Afisa Mawasiliano wa Airtel Tanzania,
Bw. Jackson Mbando, alisema kuwa Kampuni yake imekuwa na utaratibu wa
kutembelea eneo hilo la ujenzi ili kuona maendeleo yake kwa kuwa ni sehemu ya
kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususani miradi ya Afya ikiwemo
Hospitali ya Uhuru ambayo kupitia Mbia mwenza Bharti Airtel ya Tanzania ndio
iliyotoa kiasi cha Sh. bilioni 2.3 kwa Serikali ambayo ilizielekeza katika
ujenzi wa hospitali.

Alisema Kampuni ya Airtel Tanzania kwa kutambua
uhitaji wa huduma ya Mawasiliano, tayari imefungua maduka manne Wilayani
Chamwino likiwemo eneo la Hospitali ya Uhuru ambayo yataendelea kutoa huduma
ikizingatiwa kuwa baadaya ya hospitali kuanza kufanya kazi huduma za fedha
zitahitajika.

Akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa Kampuni
ya Airtel Tanzania ikitoa Gawio kwa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James alisema kuwa, Serikali ya Tanzania ilianza uchunguzi wa
umiriki wa Airtel Tanzania na baadae kufanya mazungumzo na Kampuni mama ya
Bharti Airtel ya India kuanzia mwaka 2018 na kufanikisha Serikali kumiliki
asilimia 49 ya hisa za kampuni hiyo.

Alisema makubaliano hayo yaliyosababisha kunufaika kwa
pande hizo mbili ndiyo yalimfanya Mwenyekiti wa Bharti Airtel ya India, Bw.
Sunil Mittal kutoa Sh. bilioni 2.3 kwa Serikali ikiwa ni shukrani kwa kuanza
makubaliano mapya yenye tija.

Katibu Mkuu Bw. Doto James, alisema kuwa Serikali
iliona vema fedha hizo zipelekwe kujenga hospitali ya Uhuru Mkoani Dodoma
ambayo inatarajiwa kumalizika mwezi Oktoba mwaka huu.