……………………………………………………………………
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Ikungi kimezindua kampeni zake katika jimbo la Singida Mashariki kwa kishindo huku kikisema hakina shaka na mgombea ubunge wa jimbo hilo Miraji Mtaturu kutokana na uwezo alionao kiutendaji.
Mtaturu amepitishwa na Chama hicho kuomba ridhaa tena ya kuwa mbunge baada ya kudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha takribani miezi tisa katika bunge lililopita.
Akizindua kampeni hizo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Juma Kilimba alisema CCM haikukosea kumteua Mtaturu kuwa mgombea wa jimbo hilo kutokana na kwamba anawajua vyema wananchi wake na katika kipindi kifupi alichokuwa mbunge mengi ameyafanya hivyo wananchi wana kila sababu ya kumchagua.
“Mmemuona Mtaturu hapa anaongea hajaandika mahali,lakini ameongea yote yanayotokana na Ilani yetu,ndio maana nawaambia CCM haikukosea kuwaletea huyu kwak uwa inajua kuwa ndie mtu sahihi anayejua shida zenu,anayesimamia matatizo yenu na niwaambie hatuna shaka nae,”alisema Kilimba.
Aliongeza kuwa, “Mtaturu alidumu kwenye ubunge kwa miezi karibu tisa lakini aliyoyafanya ni sawa na mtu aliyekuwa bungeni kwa kipindi cha miaka mitano ,hivi huyu mkimpa miaka mitano si atafanya balaa zaidi,?”alihoji.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mtaturu amewaomba kumchagua Dr John Magufuli aliyeonyesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi.
Amesema katika kipindi Cha miaka mitano Ilani ya Uchaguzi ya 2015- 2020 imetekelezwa kwa kiwango cha juu ikiwemo kusimamia rasilimali za nchi ili kuwafaidisha wananchi wengi.
“Ndugu zanguni niwaambie kwa nia njema kabisa,uongozi haujaribiwi,tusifanye makosa,inawezekana kuna mtu wa kabila letu anagombea Urais lakini kwa sababu sisi tunataka kiongozi bora hatutaki kiongozi wa kimila basi hakikisheni tunamchagua Dr Magufuli ili alete maendeleo ya nchi yetu,”alisema.
Amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020- 2025 imesheheni matumaini makubwa kwa wananchi hivyo wakichagua CCM wategemee mambo makubwa zaidi.
“Leo tunaona shule zinaboreshwa,vituo vya afya na hospitali zinajengwa,miradi ya maji kila mahali, umeme unasambazwa na zaidi miundombinu ya barabara inajengwa lengo likiwa ni kurahisisha maisha ya watanzania,”alisema Mtaturu.
Katika mkutano huo jumla ya wanachama 28 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiongozwa na mwenyekiti wa BAVICHA Jimbo la Singida Mashariki John Sililo walirudisha kadi na kujiunga na CCM kutokana na kuchoshwa na maneno na ahadi zisizotekelezeka ikiwemo kushinikizwa kuandamana kila wakati.