Baadhi ya wawakilishi wa wafugaji wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati (hayupo katika Picha) wakati akifungua kikao cha siku moja cha kusikiliza kero zao jana.Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati akifungua jana kikao cha siku moja cha kusikiliza kero mbalimbali za wafugaji. Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati (mwenye suti nyeusi waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja jana na wawakilishi wa wafugaji kutoka Wilaya ya Igunga mara baada ya kikao cha kusikiliza kero zao.
*************************************
NA TIGANYA VINCENT
WAFUGAJI Mkoani Tabora waliotozwa tozo zisizohalali na kupewa stakabadhi zilizoandikwa kwa mkono wametakiwa kujitokeza na kuzileka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili wahusika wachukuliwe hatua kwa tuhuma za kuwaibia.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati wakati wa mkutano kusikiliza kero mbalimbali za wafugaji kutoka Halmashauri zote.
Alisema Serikali ya Mkoa wa Tabora haiwezi kuendelea kukubali kuona wafugaji wanatozwa tozo zinazowaumiza na zinazotolewa kwa njia ya kificho na mara nyingi katika maeneo ya porini ambako hakuna mtandao wala Benki.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema tozo hizo na zile zinadaiwa kuwa zoto za meza zinatozwa na Watendaji wa Vijiji na Kata kama tozo ya Meza hizo zote ni rushwa , lazima ikomeshwe.
Dkt.Sengati aliwaomba wafugaji wote ambao wameumizwa na tozo zisizo rasmi washirikiane na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa kutoa taarifa kwa ajili ya kuwatafuta na kuwakamata wahusika wote ili waweze kurejesha fedha za walizochukua.
Alisema kama wamefanikiwa kurejesha fedha za wakulima wa tumbaku ambao walikuwa wamedhulumiwa na viongozi wasio waaminifu hawawezi kushindwa kurejesha fedha za wafugaji.
Aidha Dkt. Sengati ameagiza misako yote dhidi ya mifugo ni lazima ipate kibali kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kuzuia wafugaji kunyanyaswa.
Alisema lengo kutaka kuzuia tozo ambazo haziko katika utaratabu unaokubalika ili kuhakikisha mfugaji anaendesha shughuli zake kwa amani na utulivu bila kuvunja sheria.
Mfugaji kutoka Kipili ,Wilaya ya Sikonge Mwita Sumaku alisema ng’ombe wake 169 walikamatwa akatozwa shilingi milioni 5 , lakini stakabadhi aliyoandikiwa ilionyesha milioni 2.
Alisema alipojaribu kuwauliza wahusika walisema kuwa akiendelea atapata matatizo zaidi.
Mfugaji mwingine kutoka Sikonge Moga Maganga alisema ng’ombe wake 84 walikamatwa na kutozwa shilingi milioni 6 ambapo aliandikiwa stakabadhi ya mkono na sio ya kielektoniki kama Serikali inavyoagiza.