**************************************
Na. Majid Abdulkarim, Mpwapwa
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima ameipongeza Serikali ya Kijiji cha Kitati kilichopo katika Halmashauri ya Mpwapwa Mkoani Dodoma kwa kushirikiana vema na wananchi wa kijiji hicho na wataalamu wa afya katika halmashauri hiyo na kuwezesha kwa ufanisi utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa vyoo bora kwenye kaya.
Pongezi hizo amezitoa jana alipotembeleza kijiji hicho kilichopo takribani Kilomita 170 toka mjini Dodoma katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miundombinu bora ya vyoo kwenye Kaya za Halmashauri ya Mpwapwa inayotekeleza mpango maalumu wa WASH (Water, Sanitation and Hygiene).
Dkt. Gwajima amesema, kwa kujenga vyoo hivyo wakazi wa kijiji cha Kitati wamejitendea haki katika kusukuma maendeleo yao kiuchumi na kiafya kwani upo uhusiano wa moja kwa moja wa maendeleo ya miundombinu hiyo na uchumi wa kaya, mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Hii ni kwa kuwa fedha na muda ambao ungetumika kuwatibu watu ambao wangeathirika na magonjwa yatokanayo na uchafu kwa kukosa vyoo bora sasa watatumia raslimali hizo kwa ajili ya shughuli za maendeleo yao na taifa kiuchumi”, ameeleza Dkt. Gwajima.