Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Kitati wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma
Muonekano wa Zahanati ya Kitati iliyokamilika tangu mwaka 2019
Wananchi wa Kijiji cha Kitati wilaya ya Mpwapwa wakimfatilia kwa makini Naibu Ktatibu Mkuu TAMISEMI , Dkt. Dorothy Gwajima(HAYUPO PICHANI) alipokwa akizungumza nao
………………………………………………………..
Na. Majid Abdulkarim, Mpwapwa
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima ametoa siku 14 kwa Timu za Afya Mkoa wa Dodoma na Halmashauri ya Mpwapwa kuhakikisha Zahanati ya Kitati inaanza kutoa huduma ili kuwaondolea adha wananchi hususan huduma za kliniki na kujifungua kwa akinamama wajawazito na kliniki za chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano wasitembee mwendo mrefu kufuata huduma hizo.
Agizo hilo amelitoa jana wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miundombinu bora ya vyoo kwenye Kaya za Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma inayotekeleza mpango maalumu wa WASH (Water, Sanitation and Hygiene).
Aidha Dkt. Gwajima ameelekeza Zahanati hiyo ambayo ilikamilika tangu Disemba, 2019 iliyo takribani kilomita 50 toka Hospitali ya Halmashauri kuanza kutoa huduma kwa wakazi wa Kijiji hicho cha Kitati ili kuwasogezea huduma karibu na kuepusha wananchi kutumia fedha na muda pasipo lazima badala ya kutunza raslimali hizo na kuzielekeza kwenye shughuli zingine za maendeleo.
“Kuna wataalamu flani miongoni mwetu hawatimizi majukumu yao kwa weledi bila hata sababu ya msingi maana hata ukiwauliza sababu gani hasa hata wao wenyewe wanakosa majibu. Wataalamu hao tutawashughulikia kikamilifu ili ama watekeleze wajibu wao au wapishe wengine wenye moyo, nia na ari ya kazi za kuhudumia wananchi bila kusubiri mutu awasukume”, amesisitiza Dkt. Gwajima
Dkt. Gwajima pia amemuagiza Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya TAMISEMI, Dkt. Chaote kuwaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kutoa taarifa za Zahanati zilizokamilika na zikiwa zimeanza kutoa huduma za msingi na siyo hazitumiki kama hii ya Kitati.
Kwa kuongezea Dkt. Gwajima ameeleza kuwa huduma ya Zahanati inaweza kuanza na huduma za Kliniki ya Mama na Mtoto na kujifungua wakati huduma zingine zikiendelea kupanuliwa kwa kadri raslimali zinavyopelekwa kama ilivyopangwa kwenye bajeti na siyo kuyaacha majengo hayatumiki wakati raslimali za kuanzia zipo.
Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima ametoa Siku saba kwa Watendaji wa Hospitali ya Halmashauri ya Mpwapwa kutoa maelezo na mkakati walionao kwa ajili ya kurejesha huduma ya kichomea taka baada ya kupata hitilafu ambayo kimsingi inatengenezeka.
Vilevile, Dkt. Gwajima amewapa siku zingine 14 timu ya afya ya Halmashauri (CHMT) kuwasilisha mpango wa kila zahanati kujenga shimo la kondo la nyuma (placenta pit) kwa gharama nafuu ambayo inakadiriwa kutozidi shilingi za kitanzania laki tano kwa Force Account kama walivyofanya wengine.