Home Mchanganyiko TCRA YATOA ANGALIZO KWA VYOMBO VYA HABARI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

TCRA YATOA ANGALIZO KWA VYOMBO VYA HABARI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

0

Na Magreth Mbinga

Mamlaka ya mawasiliano Tanzania TCRA imevitaka vyombo vya habari nchini kufuata kanuni na sheria ambazo zimewekwa ili kuepusha uvunjifu wa amani nchini hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

Hayo yamezungumzwa leo na Mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo ya mawasiliano Ndg James Kilaba katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.

Pia amesema wametoa leseni kwaajili ya kuhabarisha na kuelimisha na sio vinginevyo na watakao enda kinyume na sheria ambazo zimewekwa hatua dhidi yao zitachukuliwa.

“TCRA mwezi July ilikutana na vyombo vya habari kwaajili ya kutoa elimu ya utangazaji wa habari za uchaguzi lakini kuna vituo havifuati au vinapuuzia masharti ya leseni ” amesema Kilaba.

“Mnamo tarehe 26 agosti 2020 kati ya saa 01:00 hadi saa 04:00 asubuhi kupitia vipindi vya clouds 360 na cha Power Breakfast vya Clouds TV na Clouds Radio vilirusha takwimu za wagombea wa Ubunge waliopita bila kupingwa, huku taarifa hiyo ikiwa haijathibitishwa na Tume ya Uchaguzi na kukosa mizania” amesema Kilaba.

Vilevile Kilaba amewataka wamiliki wa vyombo vya habari pindi tu leseni zao zinapoelekea kuisha wanatakiwa kuomba tena mwaka mmoja kabla ya kuisha.

Sanjari na hayo Kilaba amesema imejidhihirisha wazi kuwa vituo vingi vya utangazaji vina leseni lakini hawasomi masharti ya leseni hizo na kuhakikisha uhai wa leseni zao.