……………………………………………..
~ Ni ya kujenga Bweni, Madarasa na vyoo kwa ajili ya kuanzisha kidato cha tano na cha sita
~ Afisa Tarafa atembelea miradi hiyo
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Mapema mwezi Mei, 2020 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli alitoa fedha Tsh. Milioni 126,600,000/= kwa ajili ya kujenga Bweni, Madarasa na matundu ya vyoo ya kisasa kwa ajili ya kuanzisha kidato cha tano na cha sita kwenye shule ya sekondari ya Kitama Day.
Tangu nchi yetu ipate Uhuru Tarafa ya Mihambwe kwa mara ya kwanza kupitia shule ya Serikali hiyo ya sekondari itakuwa na Madarasa ya elimu ya juu ya sekondari ambapo kiwilaya itakuwa ya pili.
Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu alipata fursa ya kutembelea miradi hiyo ambapo alitembelea eneo litakapojengwa bweni hilo pamoja na kujionea maendeleo ya ujenzi wa Madarasa na vyoo.
Akizungumza wakati alipotembelea miradi hiyo, Gavana Shilatu alimpongeza Rais Magufuli kwa kutoa fedha hizo ambazo zitakuwa mkombozi wa kuongeza fursa ya upatikanaji wa elimu ya juu ya sekondari ambayo awali ilikuwa inapatikana mbali.
“Rais Magufuli ni wa vitendo zaidi, si tu anatoa elimu bure bali pia anaboresha miundombinu ya upatikanaji wa elimu ya uhakika kila mahali, tunamshukuru sana kwa kutuletea fedha za kujenga madarasa, vyoo na bweni. Tunamuhaidi majengo haya kukamilika kwa wakati na kwa thamani ya juu na ya ubora zaidi.” Alisema Gavana Shilatu.
Katika ziara hiyo Gavana Shilatu aliambatana na Watendaji wa vijiji, Mwalimu Mkuu pamoja na kamati ya ujenzi miradi hiyo.
Ujenzi huo unatarajia kukamilika mapema mwezi Oktoba utakuwa mkombozi kwa wakazi wa Tarafa ya Mihambwe, Tarafa jirani na wilaya kwa ujumla.