Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MGOMBEA ubunge wa jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, kwa tiketi ya CCM Christopher Ole Sendeka (Simba wa Manyara) amesema kero ya wadau wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani kupanga foleni ili wapite kwenye lango la ukuta unaozunguka migodi ya madini hayo pindi walitoka ndani inapaswa kupatiwa ufumbuzi.
Ole Sendeka ameyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni ya uchaguzi wa CCM mji mdogo wa Mirerani ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Amesema wadau wa madini ya Tanzanite wanakuwa na wakati mgumu pindi wakitoka migodini kwani kuna maeneo mawili pekee ya kukaguliwa.
Amesema kuwa watu zaidi ya elfu 10 kuwa na sehemu mbili pekee za wanaume na wanawake kupekuliwa kwa siku moja hazitoshi.
“Tunaomba mheshimiwa Waziri Mkuu ufikishe salamu zetu kwa Rais John Magufuli juu ya ombi letu la kutuongezea sehemu ya upekuzi,” amesema Ole Sendeka.
Amesema endapo maeneo ya upekuzi yakiongezwa wadau watafanyiwa upekuzi kisha wataondoka mapema kurudi majumbani mwao.
Amesema wakati mwingine mistari miwili ya kupekuliwa inakuwa mirefu hivyo wadau wa madini husimama kwa muda mwingi kusubiri kupekuliwa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema anachukua suala hilo na kukifikisha kwa Rais Magufuli ili waweze kuona jambo la kufanya.
“Ninyi cha kufanya ni kuhakikisha mgombea wetu Rais Magufuli anapata kura nyingi za kishindo kwa maslahi mapana ya wananchi ili kushughulikia hilo,” amesema Majaliwa.
Mgombea udiwani wa Kata ya Endiamtu, Lucas Chimbason Zacharia, amewaomba wananchi wa eneo hilo kumpa kura nyingi za ndiyo ili ashike nafasi hiyo.
“Kwa pamoja tutafanikiwa kufanikisha maendeleo yetu sisi wananchi hivyo tusifanye makosa Oktoba 28 mwaka huu katika kupiga kura,” amesema.