Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akifafanua jambo kwenye kikao cha Baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) iliyofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki waliohudhuria kikao cha Baraza la wafanyakazi la Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) , wakifuatilia jambo kwa makini iliyofanyika jijini Dodoma .
Mtendaji mkuu wa wakala wa ufundi na umeme (TEMESA) Eng. Japhet Masele akifafanua jambo katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) iliyofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mara baada ya kufungua kikao cha Wakala huo jijini Dodoma.
PICHA NA WUUM
…………………………………………………………………
Katibu Mkuu Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, amewataka wafanyakazi wote na Menejimenti ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kufanya kazi kwa ubunifu na weledi ili kumudu ushindani ulipo katika soko la huduma wanazozitoa nchini.
Akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi katika ukumbi wa VETA jijini Dodoma Arch. Mwakalinga amesema lazima TEMESA izaliwe upya na kufanya kazi kwa tija kwa sababu Serikali inawawezesha katika nyanja zote.
“Hakikisheni malalamiko yote ya wananchi katika ukusanyaji mapato, huduma za vivuko, ununuzi wa vipuri na utengenezaji wa magari, mnayajadili kwa uwazi na kuyapatia ufumbuzi leo hii”, amesema Arch. Mwakalinga.
Katibu mkuu Mwakalinga, amewataka TEMESA kuanzisha karakana katika maeneo yenye mahitaji makubwa ya huduma za utengenezaji wa magari na kuangalia uwezekano wa kujenga chelezo kitakachohudumia vivuko vinavyotoa huduma katika Ziwa Victoria ili kupunguza gharama.
“Mafanikio yote mtayapata endapo mtazingatia umuhimu wa kuwajali wafanyakazi katika maslahi yao na kuwashirikisha katika mipango yote ya maendeleo inayobuniwa na Menejimenti”, amesisitiza Mwakalinga.
Amemtaka Mtendaji Mkuu wa TEMESA kutoa elimu ya kutosha kuhusu rushwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ili kuhakikisha hadhi ya TEMESA inakuwa ya kupigiwa mfano.
Naye, Mtendajki mkuu wa TEMESA, Eng. Japhet Masele, amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa TEMESA imejipanga kuondoa changamoto na malalamiko yaliyokuwa yanajitokeza kipindi kilichopita kufuatia kuwezeshwa kikamilifu na Wizara katika mahitaji yake ikiwemo mishahara, posho na vitendea kazi.
Ameiomba Serikali kuunda mfuko wa kuhudumia magari ya Serikali ili kuisaidia TEMESA kukabiliana na changamoto ya kudai madeni mengi kutoka taasisi za Serikali.
Zaidi ya wataalamu 100 wa TEMESA wanakutana jijini Dodoma kutathmini kwa kina namna ya kukabiliana na changamoto za Wakala huo na hivyo kuiwezesha TEMESA kufanya kazi kwa kina na ufanisi na hivyo kuleta maendeleo kwa Taifa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.