…………………………………………………………………………
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ilemela kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt Angeline Mabula ameahidi kushirikiana na Serikali kulinda maslahi ya wafanya kazi kwa kuhakikisha anatengeneza mazingira rafiki ya biashara na kutatua kero za muda mrefu kwa watumishi wa Umma ndani ya jimbo hilo.
Dkt Angeline Mabula amebainisha hayo wakati akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano wa kampeni wa kuomba kura na kunadi wagombea wa Chama Cha Mapinduzi kwa nafasi za udiwani, ubunge na uraisi uliofanyika katika viwanja vya Nyakato Sokoni ambapo amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali ya CCM ilifanikiwa kutatua kero mbalimbali kwa wafanyabiashara wake ikiwemo kufuta kodi zisizo za msingi, kuweka mazingira rafiki ya biashara kwa kuruhusu uwekezaji mdogo na mkubwa katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi, utoaji wa mikopo ya ujasiriamali, utoaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo ili waweze kufanya biashara zao bila usumbufu wowote na uboreshaji wa masoko kwa kujenga mapya na kuboresha yale ya zamani huku upande wa watumishi wa Umma kwa jimbo la Ilemela wakikopeshwa viwanja ambapo zaidi ya walimu na watumishi wa sekta ya afya 300 wakinufaika na mpango huo, kushughulikia kero ya upandaji madaraja, ujenzi wa nyumba kumi na mbili za askari wa jeshi la polisi kata ya Nyamhongolo na ujenzi wa nyumba za walimu shule za msingi na sekondari ikiwemo shule ya Nyamadoke
‘.. Ili wafanyakazi wetu waweze kufanya kazi vizuri, wana Ilemela, wana Nyakato ni lazima tujali maslahi yao, Wenzetu wa polisi wamejengewa nyumba kumi na mbili, nyumba sita zinaendelea kujengwa, Lakini nyumba za walimu zinakwenda kujengwa ..’ Alisema
Akimkaribisha mgombea ubunge huyo, katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Bi Aziza Isimbula akawaomba wananchi hao kukiamini chama chake na kukipigia kura siku ya Oktoba 28, 2020 ili kiweze kuunda Serikali itakayowatumikia na kuwaletea maendeleo.
Nae mgombea ubunge wa viti maalum kundi la wanawake wa mkoa wa Mwanza UWT Bi Furaha Matondo akawaomba wananchi waliojitokeza katika mkutano huo kumlipa kura za NDIO mgombea wa nafasi ya Uraisi wa chama hicho Dkt John Magufuli kwa ujenzi wa miradi ya kimkakati iliyonufaisha mkoa wa Mwanza ikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza, ununuzi wa ndege za kisasa, ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa meli na vivuko ndani ya Ziwa Viktoria bila kusahau wagombea ubunge na udiwani ili iwe rahisi kwa viongozi hao kufanya kazi ya pamoja kuharakisha maendeleo.