Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Makidi wilayani Siha, Septemba 8, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
********************************************
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wasichague viongozi kwa kutumia vigezo vya udini, ukabila, itikadi za vyama na badala yake wachague viongozi watakaokuwa tayari kushirikiana nao katika kuboresha maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumanne, Septemba 8, 2020) wakati akimuombea kura Rais Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Hai, Saasisha Mafuwe na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Masama Kusini kwenye uwanja wa Kwa Sadala wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro.
“Ndugu zangu Watanzania, ndugu zangu wanaHai na wanaKilimanjaro mnatambua uwezo na uelewa mkubwa alionao Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli wa kutambua na kuona nini Watanzania wanahitaji, nawaomba siku ya kupiga kura itakapofika tujitokeze kwa wingi bila kujali itikadi zetu tumpigie kura nyingi ili akaendeleze miradi ya maendeleo aliyoianzisha.”
Amesema wakati umefika kwa wakazi wa Hai kuchagua kiongozi mwenye kujali na kutambua changamoto zinazowakabili katika maeneo yao na kushirikiana nao katika kuzitafutia ufumbuzi na kamwe wasikubali kupiga kura kwa ushabiki au kufuata mkumbo. “Mchague Rais Dkt. Magufuli kwa nafasi ya urais na Saasisha nafasi ya ubunge pamoja na wagombea udiwani wote wa CCM.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Dkt. Magufuli ni kiongozi anayetokana na Chama Cha Mapinduzi chenye utaratibu wa kuratibu miradi yote inayotakiwa kutekelezwa katika maeneo yote nchini kupitia ilani ya uchaguzi na kina mipango mizuri ya kuboresha maendeleo ya wananchi.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo kupitia mradi mkubwa wa maji unaojengwa kwa sh. bilioni 520 kutoka Machame hadi Arusha. Visima vimekamilika kuchimbwa na usambazaji wa mabomba umeanza.
“Katika mradi huu wananchi wa Hai walio katika kilomita 12 kushoto na kulia kando kando ya maeneo ambayo bomba la maji litapita tutahakikisha Mamlaka ya maji AWSA inaweka matanki kwa ajili ya kusambaza maji kwa wananchi katika ukanda wa chini.”
Amesema sh. bilioni 3.3 zimetumika kukamilisha mradi wa ujenzi na upanuzi wa skimu ya maji LOSAA – KIA. Maeneo yanayonufaika ni pamoja na kata ya Masama Magharibi, Masama Kati, Masama Kusini na kata ya KIA.
Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. milioni 844 zimetumika kukamilisha ukarabati na ujenzi wa mifereji ya maji katika skimu za Nsanya, Musa Mwinjanga na Kikavu Chini. “Skimu ya Uroke – Bomang’ombe imekamilika na inahudumia maeneo ya Machame Uroki, Kwa Sadala, Kware, Romu na Mji wa Hai.
Kwa upande wao, wananchi walisema watahakikisha wanawachagua wagombea wa CCM kwa sababu katika kipindi cha miaka 15 walichokuwa wakichagua viongozi wa upinzani hakuna kitu chochote walichokifanya cha maendeleo katika wilaya yao.
Miongoni mwa wananchi hao Betha Massawe amesema Rais Dkt. Magufuli amefanya mambo mengi ya maendeleo ikiwe kufufua usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam hadi Arusha usafiri ambao ulisimama kwa miaka 30 jambo ambalo hadi leo haamini anaona kama ndoto.
Mkazi mwingine wa Hai, David Kiseyi amesema katika uchaguzi wa mwaka huu wamejipanga kuchagua viongozi kutoka Chama Cha Mapinduzi kwa sababu wamekuwa wakiwachagua viongozi wa upinzani bila ya faida yoyote. “Rais Dkt Magufuli ameonesha upendo mkubwa kwetu kwa kutuletea miradi ya maendeleo kwetu sasa tunakwenda kuacha ushabiki na tutachagua viongozi watakaotuletea maendeleo. Watu wa Hai tuache ushabiki tuchague maendeleo.”
“Huyu Mbunge ametufanya sisi kama watoto anakuja tunampa kura kwa ahadi zake nyingi na anapopata hutumuoni tena anakimbilia Dar es salaam na Dodoma utafikiri wananchi wa huko ndio wamemchagua sasa hatupo tayari kudanganywa na maneno ya uongo ni bora akaanza kukusanya virago vyake” alisema Halima Mushi mkazi wa Machame.