*****************************
NA WILLIAM SHECHAMBO, Sengerema
MGOMBEA wa kiti cha Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema wananchi wa wilaya za Misungwi na Sengerema mkoani Mwanza, wajiandae kwa maendeleo makubwa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo ya Serikali ya CCM.
Amesema kufuatia utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa daraja la kisasa la Kigongo- Busisi, linalogharimu takriban sh. bilioni 700, Serikali yake kwa miaka mitano ijayo itahakikisha wananchi maeneo hayo wananufaika.
Dk.Magufuli alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti mkoani Mwanza jana, wakati akiomba kura za urais, ubunge na udiwani kwa wananchi wa wilaya za Misungwi na Sengerema, alipozungumza nao akiwa njiani kwenda mkoani Geita.
Alisema mradi huo hata kabla ya kukamilika, upo uhakika kuwa utafungua ukuaji wa uchumi wa wilaya hizo mbili, ambazo kisoko zitakwenda kutanua mtandao wake wa biashara kati ya Tanzania na nchi jirani ikiwamo Rwanda, Burundi na Congo DR.
“Ndugu zangu, nyie jiandae tu, kuweni tayari kwa mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwenye maeneo yenu,” alisema.
Alisema kwa kuanzia, wananchi wanatakiwa kuchangamka fursa za ajira za muda mrefu na muda mfupi, zitakazopatikana kwenye utekelezaji wa kila hatua wa mradi huo, ambao fedha zake zote, zimetokana na mapato ya ndani.
“Kama ni Mama Lishe, pika chakula, watu wafanye kazi na niwaambie hili mnaloliona sasa linajengwa ni la muda tu, kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kazi, daraja lenyewe linakuja.
“Litakuwa daraja refu zaidi Afrika Mashariki kwa urefu wa kilomita 3.2 na la sita kwa urefu Afrika, niwahakikishie hapa tutapageuza na kuwa kama Ulaya, watalii watakuja hapa, daraja hili litakuwa la kipekee,” alisema Dk. Magufuli akiwa Busisi.
Akiwa Sengerema, Dk. Magufuli alisema daraja hilo la Kigongo- Busisi, litaiinua wilaya hiyo ambayo amebahatika kuifahamu kwa miaka mingi, kwa sababu aliishi hapo miaka ya 1980 kama mtumishi wa umma.
“Daraja hili ndio litautengeneza mji wa Sengerema, ninawaambia ukweli, kwa sababu litakapokamilika nyumba zitaungana kutoka Sengerema mpaka Busisi, biashara zitakuwa.
“Na kwa bahati nzuri daraja hili halitakuwa la CCM tu wana CUF watapita, Chadema nao watapita, ACT watapita, NCCR Mageuzi watapita, kwanini mninyime kura?,” alisema.
Dk. Magufuli alisema kuhusu ombi la mbunge mtarajiwa wa jimbo hilo, Hamis Tabasamu, kuhusu uhitaji wa lami kutoka Sengerema- Katunguru mpaka kivuko cha Kamanga atalitimiza, kwenye kipindi cha pili cha uongozi wake.
“Ninataka hapa pawe na Soko, mtu akinunua bidhaa zake aamue aite njia gani rahisi kwake, ikiwemo hii ya Katunguru- Kamanga atokezee Mwanza mjini.
“Leo Septemba 8, naahidi mkimchagua tu mbunge wenu (Hamis Tabasamu), anikumbushe nitaijenga hii barabara yenye urefu wa kilomita 34.93 kwa kiwango cha lami,” alisema.
Alisema kwa miaka mitano iliyopita, Serikali imefanya miradi ya maji yenye gharama ya sh. bilioni 27.2 wilayani Sengerema, ukiwemo wa Sengerema- Buchosa, unaogharimu sh. bilioni 3.8.
“Mambo ni mengi tuliyoyafanya kwenye elimu, afya kila mahali, ndio maana tunaomba tumekuja kuomba tena kura, tumalizie tuliyoyaanza,” alisema.
AWAONYA WAKULIMA
Dk. Magufuli akizungumza kuhusu mchango wa Serikali kwenye kilimo wilayani Sengerema alisema Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), pamoja na mambo mengine imewakopesha wakulima wilayani humo matrekta tisa.
“Nafahamu mmevuna vizuri mwaka huu, nawaomba msiuze mazao yenu kwa pupa, muyatunze na hata mkiuza muuze wa bei nzuri lakini ni jukumu letu kutunza chakula, tusije tukafa njaa,” alisema.
Mgombea huyo alisema anatoa wito huo kutokana na hali ya uhitaji mkubwa wa chakula iliyopo duniani kwa sasa, kutokana na janga la covid-19.
Awali, Mbunge wa Sengerema, Tabasamu, alisema wananchi wa jimbo hilo watarudisha fadhila kwa Dk. Magufuli, Oktoba 28, kutokana na mengi aliyowafanyia ikiwemo kuwajengea hospitali ya wilaya.
“Kwa miaka 45 hatujawahi kuwa na hospitali ya wilaya, lakini wewe ndani ya miaka mitano umetujengea tunashukuru sana, fadhila za wananchi 42,000 zitalipwa Oktoba 28,” alisema.
Kadhalika alisema wanaomba Sengerema ipewe hadhi ya mji kwa sababu ni muda ni sasa haujapandishwa hadhi na kuwa halmashauri ya mji, kama ilivyo kwa miji mingine ambayo ilianzishwa kipindi kimoja ukiwemo Korogwe, Bariadi, Masasi na Tarime.
Alisema ombi lingine kutoka kwa wana Sengerema ni lami kwenye halmashauri hiyo na kwamba ufungaji wa taa za barabarani uko ndani ya uwezo wa mbunge huyo.
UNDANI DARAJA LA BUSISI-KIGONGO
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale, wakati wa uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo, alisema ujenzi huo ukijumuisha barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.66 umepangwa kukamilika Julai mwaka 2023.
Alisema daraja hilo refu kuliko yote Afrika Mashariki na la 6 kwa urefu Barani Afrika litakuwa mbadala wa vivuko vya MV Misungwi, MV Sengerema na MV Mwanza.
Mfugale alisema litajengwa kwa teknolojia ya madaraja marefu inayoitwa ‘Extra Dosed Bridge’ ambapo litajengwa juu ya nguzo 67 zikiwemo nguzo 3 zenye urefu wa meta 40 na umbali wa meta 160 kutoka nguzo moja hadi nyingine.
Mhandisi Mfugale amebainisha kuwa daraja hilo linalojengwa na wakandarasi China Civil Engineering Construction Corporation na China Railway 15 Group Corporation litaondoa adha ya usafiri wa wananchi, mizigo na magari ambayo kwa sasa huvushwa kwa vivuko.
Alisema baada ya ujenzi idadi ya magari yanayovuka kwa siku inatarajiwa kuongezeka kutoka 1,600 hadi 10,200 kwa siku na muda kuvuka utapungua kutoka saa 2:30 hadi dakika 4.
Kwa upande wake Dk. Magufuli katika hafla hiyo, aliwapongeza wananchi wa Kanda ya Ziwa hususan Mikoa ya Mwanza na Geita kwa ujenzi wa daraja hilo.
Alisema litakapokamilika litakuwa utatuzi wa kudumu wa kero ya miaka mingi, iliyosababisha vifo kutokana na ajali za majini na wagonjwa kucheleweshwa hospitali, kuchelewa kwa biashara na safari za wananchi.
Leo, Dk. Magufuli anaendelea na mikutano yake ya Kampeni mkoani Geita kwa kufanya mkutano katika viwanja vya Busolwa, mjini Geita.