Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya wiki moja ya mbinu za utafiti kwa wataalamu wa kada mbalimbali yaliyofanyika hospitalini hapa.
Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi SAhirikishi Muhimbili-MUHAS, Prof. Method Kazaura akiwasilisha mada.
Wataalamu wakifuatilia kwa makini mada katika mafunzo hayo.
Dkt. Magandi katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.
…………………………………………………………..
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imefungua mafunzo ya wiki moja kwa washiriki 25 wa kada mbalimbali yanayolenga kuwapa ujuzi wa mbinu za utafiti ili kuboresha utoaji huduma za afya kwa watanzania.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema kuwa uongozi wa hospitali ya Muhimbili Upanga na Mloganzila unaunga mkono mafunzo ya wataalamu mahali pa kazi kwani yatasaidia kuboresha utoaji huduma.
“Napenda kusisitiza kuwa bodi ya wadhamini na uongozi wa MNH tunaunga mkono ufanyaji wa tafiti hizi kwa maslahi mapana ya taifa letu na maboresho ya utoaji huduma za afya katika hospitali yetu.” Amesema Dkt. Magandi.
Sambamba na hilo Dkt. Magandi ameeleza kuwa ili kuweza kufikia mapinduzi makubwa katika sekta ya afya hatuna budi kujikita katika ufanyaji wa tafiti mbalimbali kama ilivyo katika nchi zilizoendelea kama vile Marekani, Uingereza, China na Afrika ya Kusini ambazo ni baadhi tu ya nchi zinazofanya tafiti nyingi na kuleta matokeo chanya katika sekta ya afya.
Aidha Dkt. Magandi ametaja moja ya faida za utafiti kuwa ni pamoja na kuwasaidia watafiti na wataalamu wa afya katika kada zote kupata njia mpya na sahihi za kuelewa, kugundua, kudhibiti na kutibu maradhi mbalimbali ya binadamu.
Mafunzo hayo yataendeshwa na wataalamu bobezi katika tafiti za afya kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili- MUHAS kwa kusimamiwa na Kitengo cha Elimu, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu MNH-Mloganzila.